Na Allan Vicent, Tabora<timesmajiraOnline, Tabora
SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imepongezwa kwa kumwaga mabilioni ya fedha katika Mkoa wa Tabora kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwemo kuboreshwa sekta ya afya katika wilaya zote.
Pongezi hizo zilitolewa na Kaimu Mkuu wa Mkoa huo ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Uyui Zakaria Mwansasu katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika jana katika ukumbi wa Mtemi Isike Mwanakiyungi.
Alisema kuwa Mkoa huo unajivunia kupata mafanikio makubwa katika sekta za elimu, afya, barabara, maji, nishati na uwezeshaji wananchi kiuchumi katika kipindi cha miaka 3 ya utawala wa Rais Samia.
Mwansasu alibainisha kuwa sekta ya afya ni miongoni mwa sekta zilizokuwa na changamoto nyingi lakini Mheshimiwa Rais ameleta zaidi ya bil 29 kwa ajili ya utekelezaji miradi ya afya ili kuboresha huduma za matibabu kwa wananchi.
Alifafanua kuwa fedha hizo zimetekeleza miradi mbalimbali katika halmashauri zote 8 ikiwemo kujengwa Hospitali za Wilaya, Vituo vya Afya, Zahanati na kununua vifaa tiba na madawa.
‘Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwafanyia mambo makubwa wakazi wa Mkoa wa Tabora ikiwemo kuboreshwa huduma za afya mjini na vijijini’, alibainisha.
DC Mwansasu aliongeza kuwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024 hadi kufikia Desemba 2023 Mheshimiwa Rais keshaleta fedha zaidi ya nusu ya bajeti yote ya maendeleo ya Mkoa huo na miradi yote inaendelea kutekelezwa kwa kasi kubwa.
Akifafanua zaidi Mganga Mkuu wa Mkoa huo (RMO) Dkt Honoratha Rutatinisibwa alisema kuwa katika kipindi cha miaka 3 ya Mheshimiwa Rais jumla ya Hospitali 5 mpya za Wilaya zimejengwa kwa gharama za zaidi ya sh bil 10.
Aidha Vituo vya Afya 19 vimejengwa na maboma ya zahanati zaidi ya 94 yamekamilishwa na huduma za afya tayari zimeanza kutolewa huku zingine zikiwa katika hatua ya mwisho ya umaliziaji.
RMO aliongeza kuwa sekta ya afya imeboreshwa kwa kiasi kikubwa katika Wilaya zote za Mkoa huo ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo Kitete ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 imepata Mashine ya kisasa ya CT-SCAN ya sh bil 1.8.
Aidha Hospitali 6 zilizopo katika Wilaya za Kaliua, Uyui, Urambo, Sikonge, Manispaa Tabora na Igunga kila moja imepata mashine ya kisasa ya mionzi (x-ray) zilizogharimu zaidi ya sh mil 700.
Alibainisha kuwa mbali na kujengwa miundombinu hiyo Mheshimiwa Rais pia alileta zaidi ya sh bil 8 kwa ajili ya kununuliwa vifaa tiba na dawa kwa ajili hospitali na vituo vyote vya kutolea huduma za afya.
Mbali na maboresho makubwa yaliyofanyika katika sekta hiyo alitaja Hospitali mpya 5 zilizojengwa na Mheshimiwa Rais katika miaka 3 ya Utawala wake kuwa ni za Wilaya ya Kaliua, Manispaa Tabora, Sikonge, Uyui na Nzega .
More Stories
Madaktari wa Tanzania, Comoro waanza kambi kwa kishindo
Watakiwa kushirikiana kutikomeza matatizo ya lishe
CCBRT yazidi kuunga mkono juhudi za Rais Samia