Na Allan Kitwe, Timesmajira Online,Tabora
Chuo cha Tabora Network Training,kimekuwa msaada kwa vijana wa Mkoa wa Tabora kwa kutoa mafunzo ya vitendo na nadharia katika fani mbalimbali zenye uhitaji sokoni, ikiwemo TEHAMA, ujasiriamali, ufundi umeme, ualimu wa awali na ukutubi.
Mafunzo hayo yamewanufaisha vijana zaidi ya 155 kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo, pamoja na vikundi vya wajasiriamali wakiwemo wanawake, kwa lengo la kuwawezesha kuajiriwa au kujiajiri na hivyo kuinua hali zao za kiuchumi.
Akizungumza katika mahafali ya 10 ya chuo hicho, Diwani wa Kata ya Kanyenye,Zubeda Changarawe,ameeleza kuwa kazi inayofanywa na chuo hicho ni mchango wa moja kwa moja katika kuunga mkono juhudi za serikali ya za kuwawezesha vijana.
Makamu Mkuu wa Chuo,Andrea Alphael, alisema tangu kuanzishwa mwaka 2004, chuo hicho kimefanikiwa kuwafundisha vijana maelfu, wengi wao wakiwa wamepata ajira au wamejiajiri kwa kutumia maarifa waliyopewa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Chuo, Andrew Maisha,amesema taasisi hiyo itaendelea kuandaa kozi zenye tija kwa jamii na kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuendeleza juhudi za kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi.
Wahitimu waliomaliza mafunzo yao, akiwemo Isack Oscar na Rahma Kambona, walieleza kuwa elimu waliyoipata imekuwa msingi wa mafanikio yao ya kikazi na kibinafsi, huku wakilihimiza taifa kuwekeza zaidi kwenye elimu ya vitendo kwa vijana.
More Stories
Ilemela yatenga milioni 920 kwa ajili ya mikopo ya vikundi
Wanawake watakiwa kutochafuana kuelekea uchaguzi mkuu
Serikali Kuboresha Elimu ya Ufundi: Shule 55 Kubadilishwa Kuwa Sekondari za Amali