December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Dkt.Osmundi Mwanyika akifungua warsha ya siku mbili ya wawakilishi wa wazee pamoja na maafisa wa serikali

Taasisi zaombwa kuhamasisha utoaji huduma kwa wazee

Na Esther Macha, Timesmajira , Online, Mbeya  

TAASISI za kiserikali na kidini mkoani Mbeya zimetakiwa kuhamasisha uwepo wa mifuko ya kijamii ambayo itasaidia utoaji wa huduma za afya kwa wazee. 

Hayo yamesemwa na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dkt. Osmunda Mwanyika wakati wa ufunguzi wa malengo ya mkutano wa viongozi na maafisa wa serikali, wadau na wawakilishi wa wazee kuhusiana na uingizwaji wa masuala ya wazee katika mipango ya maendeleo ya halmashauri  na mkoa. 

Baadhi ya wazee wakimsikiliza Dkt Mwanyika

Dkt Mwanyika amesema kuwa wazee hawatakuwa na afya njema iwapo afya zao hazipo sawa na itakuwa ni vigumu kujishughulisha na masuala ya kijamii. 

Aidha amesema ipo haja kwa taasisi za kiserikali na kidini kuangalia bajeti zao ili kusaidia wazee katika suala la huduma za afya ambazo mara nyingi zimekuwa changamoto kwa wazee.

“Tunaomba tushirikiane kwa pamoja, taasisi zote zilizopo hapa na kwamba tukifanya hivi tutaweza kuwasaidia wazee na kuwa katika afya njema kutokana na maradhi yanayo wasumbua” alisema Dkt. Mwanyika. 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo ya siku mbili, Mkurugenzi wa KIWWAUTA, shirika lisilokuwa la kiserikali linalojishughulisha na masuala ya wazee, Amina Mwinami amesema kuwa lengo la mkutano huo ni kubadilishana uzoefu kuhusu changamoto zinazowakabili wazee na namna ya kuzikabili. 

Aidha Mkurugenzi huyo amesema anaamini kuwa mkutano huo wa siku mbili utaleta mabadiliko makubwa kwa watendaji wa serikali na kuanza kuingiza masuala ya wazee katika bajeti za halmashauri na mkoa na kupunguza changamoto zinazowakabili wazee kwa kutumia rasilimali zilizopo. 

Kwa upande wake mwenzeshaji wa warsha hiyo ambaye ni Mratibu wa KIWWAUTA, Mussa Mcharo amesema kuwa wazee bado wana changamoto ambapo asilimia 5.7 wanatunza zaidi nusu ya watoto yatima wote (sawa na watoto milioni 2).

Hata hivyo Mcharo amesema wazee wengi siyo walengwa wa miradi mingi ya ukimwi, kufiwa na waliokuwa wanawategemea, kuwa na matatizo ya kisaikolojia.