Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
TAASISI za kihabari nchini zimeieleza Serikali kuwa, mwelekeo wa Tanzania katika uhuru wa habari umekuwa si wa kujivunia katika ngazi ya Kimataifa, kwani kwa mujibu wa ripoti ya Waandishi Wasio na Mipaka inaonyesha kwa miaka mitano mfululilizo Tanzania imekuwa na anguko la uhuru wa vyombo vya habari.
Hayo yameelezwa na taasisi hizo kupitia taarifa ya pamoja iliyosomwa mbele ya viongozi mbalimbali wakiongozwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa katika Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani iliyoadhimishwa Kitaifa jijini Arusha leo.
“Wakati mwaka 2016 Tanzania ilikuwa nafasi ya 71 kati ya nchi 180 kwa Uhuru wa Vyombo vya Habari, mwelekeo umekuwa ni wa kushuka kwa kuelekea kusiko. Mwaka 2017, nchi yetu ilishuka na kuwa ya 83, mwaka 2018 ikwa ya 93, mwaka 2019, ikawa ya 118 na mwaka 2020, ikawa ya 124.
“Hili ni anguko la nafasi 53, ambalo si la kujivunia.Mheshimiwa mgeni rasmi, matukio yanayotuangusha ni pamoja na kufungia magazeti, waandishi kupigwa, redio kutozwa faini kiholela, mitandao ya kijamii kufungiwa, kesi zinazotokana na uchapishaji wa habari kufunguliwa kama jinai badala ya madai, watu kufikishwa mahakamani kwa kutoa maoni yao mtandao na mengine mengi ya aina hiyo au yanayofanana na hayo,”imefafanua taarifa hiyo ya pamoja.
Miongoni mwa wadau waliofanikisha maadhimisho hayo ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO), MISA-Tanzania, Jukwaa la WahaririTanzania (TEF), Friedrich Ebert Stiftung, Baraza la Habari Tanzania (MCT).
Pia kuna Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Tanzania Media Foundation (TMF), United Nations Tanzania, Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Nukta Afrika, Jamii Media, Elimika, Twaweza, East Africa Radio,Sikika, Jamii Forums na Legal Services Facility -LSF.
Taasisi hizo za kihabari zimetolea mfano kuwa,Aprili 21, mwaka huu mwandishi wa Gazeti la Mwananchi, Jesse Mikofu alipigwa na kuharibiwa simu yake aliyoitumia kupicha picha askari wa JKU Zanzibar, waliokuwa wanahamisha wafanyabiashara ndogo ndogo kutoka eneo la Darajani kwenda Kibandamaiti visiwani Zanzibar.
“Tunaipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa hatua ilizochukua ikiwamo kufanya mkutano na waandishi wa habari kupinga udhalimu huu, kwenda ofisi za Mwananchi Zanzibar kumpa pole na kumuomba radhi mwandishi aliyepigwa na kuwachukulia hatua askari husika. Tunasema asante sana SMZ.Pamoja na tukio hilo la Zanzibar, katika Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Lusubilo J. Mwakabibi, mara kadhaa amekamata waandishi na kuwaweka ndani.
“Tukio la karibuni liliwahusisha waandishi wa Habari wa ITV/Radio One na Island TV ambao aliwakamata na kuwaweka ndani kwa saa kadhaa.Tunaishukuru Serikali imemsimamisha kazi kupisha uchunguzi wa matumizi mabaya ya madaraka.
“Pia yapo matukio mengine kama lile la Mwandishi wa Gazeti la Nipashe mkoani Kilimanjaro, Mary Mosha kutishwa na wapambe wa Meya wa Manispaa ya Moshi, Juma Rahib, kutokana na habari aliyoandikwa chanzo chake kikiwa ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani humo.
“Mwandishi mwingine ni Janeth Joseph wa Mwananchi, ambaye mwaka 2020 alipigwa kwa kitako cha bunduki na askari wakati akiwa kazini. Mwingine ni mwandishi wa The Guardian, James Lanka, ambaye mwaka huu aliwekwa maabusu ya polisi kwa siku tatu na kunyimwa haki ya kutoa taarifa kwa ndugu ili apate dhamana.
“Lanka alikamatwa alipokuwa alifuatilia habari ya maofisa wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi kukusanya ushuru siku ya Jumalipi kwa kutumia na pasipokutoa stakabadhi.Kadhalika mwandishi Elia Peter wa Global TV alitoa taarifa za kupokea vitisho mara kwa mara kutoka kwa mmoja wa vigogo wa wilaya mojawapo ya mkoa wa Kilimanjaro, jambo ambalo limekuwa likimwogofya katika kutekeleza majukumu yake.
“Yapo pia matukio ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana –Mwanza kumtishia mwandishi wa ITVna lile la mkoani Katavi ambako wananchi walichukua sheria mkoani dhidi ya waandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten waliokuwa wamekwenda kuandika habari za uchaguzi wa Imamu wa Msikiti.
“Wale ambao hawakukubali matokeo waliamua kushambulia waandishi hao wa habari na kuharibu vifaa vyao vya kazi. Hili halikubaliki.Pamoja na kupongeza hatua ambazo zimechukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia kwa Waziri mwenye dhamana ya Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo,Tabia Maulid Mwita, na zile za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia kwa Waziri mwenye dhamana na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu.
“Sisi wanahabari tunasikitishwa na kuhuzunishwa na wimbi lililoibuka la kushambulia waandishi wa habari, kuharibu vifaa vya kazi au kuwakamata na kuwaweka ndani kwa ubabe bila kufuata misingi ya sheria.Imekuwa ni kawaida kwa baadhi ya askari ndani ya vyombo vya dola, baadhi ya wakurugenzi wa halmashauri za wilaya na wakuu wa wilaya wachache, wameanzisha vita dhidi ya waandishi wa habari wanaowakamata, kuwatesa, kuwaweka ndani na kuharibu vifaa vyao vya kazi. Hili halikubaliki.Wanahabari nchini Tanzania, tunaona mwelekeo huu unatutisha hasa tunapoona watendaji serikalini na baadhi ya askari wakiwa wamebuni mbinu ya kukamata, kupiga, kunyanyasa na kuharibu vitendea kazi vya waandishi wa habari.
“Hali hii inawatisha na kuwaogofya waandishi wa habari waache kufuatilia matukio na watendaji hawa au askari wapate fursa ya kunyanyasa wananchi watakavyo.Mwandishi wa habari ni jicho la jamii hivyo anapaswa kuwapo katika matukio karibu yote kuhakikisha wananchi wanafahamu kinachoendelea. Iwapo mtu anatenda jambo jema, hana sababu ya kuhofia uwepo wa waandishi wa habari.Hali halikubaliki kamwe na inachangia kuzorota kwa uhuru wa vyombo vya habari nchini,”wameeleza kupitia taarifa hiyo.
Wakizungumzia sheria za habari wamesema kuwa,Mahakama ya Afrika Mashariki ilitoa hukumu ikielekeza Serikali ifute vifungu tisa katika Sheria ya Huduma za Habari (MSA, 2016) kwa kuwa vinakinzana na Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Mheshimiwa Rais Samia, ameiagiza Serikali kufanya marekebisho ya sheria kandamizi ziwe katika mukutadha unaoeleweka na kutamka bayana aina ya adhabu kwa kila kosa.Serikali kupitia kwa aliyekuwa Waziri wa Habari Dkt. Harisson Mwakyembe alipokutana na Uongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na ujumbe wa International Press Institute (IPI) Aprili 2, 2019 alisema Serikali iko tayari kukutana na wadau kurekebisha upungufu kwenye sheria hii.
“Kadhalika Katibu Mkuu wa Wizara yako, Dkt. Hassan Abbas alipozungumza katika moja ya matukio ya utangulizi wa maadhimisho haya pale jijini Dar es Salaam, alisema milango iko wazi kwa mapendekezo ya kurekebisha sheria za kihabari. Ombi letu ni kwamba utekelezaji huu uwe wa haraka na usibakie kuwa ahadi tu.Mheshimiwa mgeni ramsi, kati ya sheria kandamizi zinazolalamikiwa ni pamoja na Media Services Act 2016, Cyber Crimes Act 2015, Statistics Act 2015 (kama ilivyorekebishwa 2018), Right to Information (RTI) 2016, Online Content Regulation 2017, na nyingine nyingi ambazo kwa njia moja au nyingine zinaminya uhuru wa habari au watu kutoa mawazo.
“Tunaomba hizi zirekebishwe na kuondoa masharti yanayokandamizia uhuru wa habari nchini, ikiwemo hili gumu la kutoa leseni kwa magazeti inayotumika kama fimbo vya kufumba midomo ya baadhi ya wachapishaji,”imefafanua taarifa ya taasisi hizo za kihabari nchini.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini