November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Taasisi za fedha zaombwa kuwatembelea wakulima shambani

David John, Timesmajira Online, Tabora

MKULIMA wa zao la tumbaku wilayani Sikonge mkoani Tabora Masoud Kilyamanda ameziomba taasisi za kifedha nchini kuwatembelea wakulima  katika mashamba yao kujionea uwekezaji wanaofanya ili waweze kuwakopesha.

Kilyamanda ameyasema hayo wilayani Sikonge  baada ya kutembelewa na waandishi wa habari kwenye mashamba yake  wilayani humo Mkoani Tabora..

” Ndugu waandishi wa habari kama mnavyoona wenyewe hapa ni zaidi ya hekari 300 na ningeweza kuajiri vijana zaidi ya 20 na wanalipwa mshahara hapa karibu milioni 48 hivyo ni uwekezaji mkubwa  na ndio maana nasema naishukuru taasisi ya fedha hasa Azania Benki kwa kuweza kuniamini na kunipa mkopo wa Trector,”amesema 

Hivyo ameziomba taasisi zingine kuwa karibu na wakulima hasa mkulima mkubwa kama yeye na  kuwatembelea wajionee wenyewe uwekezaji huo anaamini kuwa watakapoona kwa macho ni rahisi kumkopesha mkulima. 

Amesema licha ya kufanya vizuri kwenye kilimo cha tumbaku lakini anatamani pia kufanya shughuli za ufugaji wa samaki hivyo anaiomba serikali kupitia Wizara ya kilimo chini ya  Waziri Hussein Bashe kumusaidia ili aweze kupata malambo ya kuhifadhi maji.

Pia kilyamanda ameongeza kuwa ukichia mbali kilimo  anajishughulisha na ufugaji ambao hadi kufikia sasa ana ng’ombe 80 na  ameweza kutoa ajira Kwa vijana ambao wanamfanyia kazi huku  ndoto yake nikuwa mkulima mkubwa zaidi  na mtu ambaye ataendelea kuisaidia serikali kutatua tatizo la ajira.

Sanjari na hayo amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa  kuhakikisha kuwa sekta ya kilimo inanufaisha walengwa hususani zao la tumbaku ambalo kampuni za ununuzi wa zao hilo zimezidi kuongezeka na kilimo hicho kuonekana chenye tija.

 Amesema kuwa anamshukuru Rais Dkt Samia kwa kuruhusu kampuni za nje kuja nchini kununua zao la tumbaku jambo ambalo limewafanya wakulima waanze kuwa na maisha bora na kuendelea kuwa na imani zaidi na serikali ya awamu ya sita.

Pia amesema kama serikali itaendelea kutoa ruzuku kwenye mbolea wakulima watafanya mabadiliko makubwa sana ya kimaendeleo hasa Mkoa wa Tabora ambako zao la tumbaku linalimwa kwa wingi ukizingatia zao hilo ni zao la kibiashara na kimkakati.

Naye  mkulima mwingine wa zao la tumbaku mkoani humo Shija Madowo akizungumzia  baadhi ya changamoto zinazowakabili wakulima amesema changamoto ni kipindi wanapofikia  ukaushaji wa tumbaku kwani ili  ikauke inahitaji kuni au miti ya kuni jambo ambalo wakati mwingine linaleta shida .

Amesema kuwa wakati wakukausha tumbaku wamekuwa wakilazimika kulipia  seikalini ambapo kwa hekta moja wanalipa dola 200 za kimarekani na kuongeza kuwa badala ya kupungua gharama inazidi kuongezeka hivyo amewaomba waandishi wa habari kusaidia kupaza sauti ili serikali iweze kuwasaidia

Madowo alifafanua kuwa kilimo cha tumbaku gharama yake kubwa ni kwa upande wa mbolea ambapo mfuko mmoja ni 170,000 za kitanzania jambo ambalo kwa mkulima wa kawaida hawezi kumudu gharama hizo

.“Naiomba serikali ijaribu kuangalia kwenye changamoto za mbolea hususani tupate ruzuku ya pembejeo ya tumbaku NPK ,kwa kweli tunashukuru kwa upande wa mwaka jana tulipata ruzuku ya mbolea ya kutosha ndiyo maana kwa msimu huu tumevuna mazao ya kutosha,”amesema Mkulima huyo.

Amesema kuwa anaelekeza ombi lake kwenye Wizara ya Kilimo kutatua changamoto ya mbolea ya ruzuku ya zao la tumbaku aina ya NPK, na kutumia nafasi hiyo kumwomba Waziri Hussein Bashe awasaidie  wakulima  wa zao hilo  ili waendelee kulima kwa wingi na waweze kunufaika.