November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Taasisi yachangia wanawake wa minazi mirefu

Na Heri Shaaban, TimesMajira Online, Dar es Salaam

TAASISI ya Wahenga Aluminium imetoa Sh 500,000 kusaidia kikundi cha kikoba cha Tujijenge Pamoja kilichopo Kata ya Minazi Mirefu ili kiweze kujikwamua kiuchumi.

Mkurugenzi Mkuu wa Wahenga Aluminium, John Ryoba, alichangia fedha hizo katika harambe ya kuadhimisha miaka mitano ya kikundi hicho ambapo mgeni rasmi alikuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Kate Kamba aliyechangia Sh 100,000 na kuahidi kutoa mchango mwingine baadaye.

Akizungumza katika hafla hiyo Ryoba ambaye alikuwa mgeni maalumu alisema amekuwa akishirikiana na kikundi hicho pamoja na kuchangia shughuli mbalimbali za chama.

“Niko pamoja na ninyi na nitaendelea kuwasaidia ili mjikwamue kiuchumi kwa sababu tunaamini wanawake mnaweza,” alisema Ryoba.

Aliwataka wanachama wa kikoba hicho kushirikiana kwa pamoja ili waweze kusonga mbele na kufikia malengo yao.

Kwa upande wake mgeni rasmi Mwenyekiti wa CCM Mkoa Dar es Salaam, Kate Kamba, alisema chama kitashirikiana nao katika kutatua changamoto zao na kuwasaidia ili waweze kusonga mbele.

Msaidizi wa Mbunge wa Jimbo la Segerea, Rutha Rucharaba, alisema Kata ya Minazi Mirefu kuna vikundi vingi vya wanawake na vijana lakini havijapata mikopo inayotolewa na halmashauri.

Alisema hawajajua kinachokwamisha hali hiyo na changamoto hiyo na kuomba CCM Mkoa wa Dar es Salaam iweze kuwasaidia.

Rutha alisema awali Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonah Ladslaus Kamoli, alichangia bati 20 kwa ajili ya ofisi inayojengwa na kikundi hicho.

Wenginge waliochangia harambee hiyo ni Madiwani Wanawake wa Wilaya ya Ilal ambapo Lucy Lugome wa Kisukuru alichangia Sh100,000, Rukia Chacha (Sh 100,000) na Moza Mwano ambaye pia ni mlezi wa kikoba hicho (Sh 100,000), UWT Minazi Mirefu (50,000) na
Msaidizi wa Mbunge (Sh 30,000).

Mwenyekiti wa Kikundi cha Wanawake Tujijenge Pamoja, Hadija Magube, alisema wanakabiliwa na changamoto za viti 300, meza 60, maturubai sita, vifaa vya ofisi na umaliziaji wa ofisi yao ambapo vyote vinagharimu Sh milioni 21.4.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Wahenga Alminium John Ryoba akizungumza na Wanawake wa Kikundi Cha vikoba Tujenge Pamoja Minazi Mirefu Wilaya llala Leo Machi 12/2022 Ryoba alikuwa Mgeni Maalum katika hafla(PiCHA HERI SHAABAN)
Mwenyekiti wa CCM mkoa DAR ES SALAAM Mama Kate Kamba akimkabidhi zawadi Mkurugenzi wa Kampuni ya Wahenga Alminium John Ryoba katika hafla ya miaka mitano ya Kikundi Cha Wanawake tujijenge pamoja Minazi Mirefu Wilaya llala Leo Machi 12/2022 (Katikati) Diwani wa Viti Maalum Wanawake Moza Mwano (Picha na HERI SHAABAN)
Katibu wa Mbunge wa Jimbo la SEGEREA Rutha Rucharaba akizungumza na Wanawake wa Kikundi Cha vikoba Tujenge Pamoja Minazi Mirefu Wilaya llala Leo Machi 12/2022 Rutha alitumia fursa hiyo kuongea Kwa niaba ya Mbunge wa SEGEREA Bonah Ladslaus Kamoli (Katikati) Diwani wa Viti Maalum Wanawake Moza Mwano (kushoto) wa CCM mkoa DAR ES SALAAM Mama Kate Kamba (Picha NA HERI SHAABAN)