September 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Taasisi ya Women Tapo, Hospitali ya Aga Khan wasaini mkataba wa makubaliano

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

KATIKA kuhakikisha wanawake wanaofanya biashara masokoni na wachuuzi wanapata huduma bora za Afya, Taasisi ya Women Tapo na Aga Khan Health Service, Tanzania (AKHS, T) wamesaini mkataba wa makubaliano wa kushirikiana katika kushugulikia changamoto za kiafya kwa kinamama hao.

Ushirikiano huo unatarajia kuleta mabadiliko katika upatikanaji wa huduma ya afya kwa wanawake, wasichana na watoto wa Kitanzania.

Akizungumza wakati wa utiaji saini wa makubaliano hayo uliofanyika leo Septemba 13, 2024 jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Vituo vya Afya vya Aga Khan Tanzania, Hassan Ali amesema ushirikiano huo unalenga kuimarisha ustawi wa kiuchumi na kijamii wa wanawake hao kwa kupatiwa huduma za afya.

“Tunajivunia kushirikiana na Women Tapo, ambapo kama ilivyo utaratibu wetu wa kusaidia jamii na watu wenye hali ya chini, tukaona tutumie fursa hii kuhakikisha kina mama hawa wanapata matibabu katika vituo vyetu kwa gharama nafuu ambapo pengine angekuja mwenyewe angetumia laki moja na zaidi lakini kwa ushirikiano huu atatibiwa kwa gharama ya Sh. 40,000 tu.

“Program hii ni mtambuka, ambapo watoto wa kike na watoto wachanga wa kiume pia wapo kwenye program hii…pamoja na hayo tutatoa elimu ya afya kwa kinamama hawa ikiwemo ya masuala ya lishe, magonjwa yasiyoambukiza na yanayoambukiza,” amefafanua.

Amebainisha huduma hiyo itapatikana katika Vituo vyao vya Afya vilivyopo katika Wilaya ya Ubungo ambavyo ni Sinza na Kimara na vilivyopo katika Wilaya ya Ilala ikiwemo Town Centre, Tabata pamoja na Ukonga.

“Tunawakaribisha na wadau wengine kuweza kusapoti Taasisi hii ya Women Tapo hasa eneo la rasilimali fedha, ili kuweza kuwasaidia kina mama na watoto waweze kupata huduma bora za afya,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Women Tapo, Lulu Nyapili amesema ushirikiano huo na Aga Khan Health Service, Tanzania ni hatua ya kuleta mabadiliko kwa afya na ustawi wa wanawake wachuuzi wa Kitanzania.

“Tunawashuru sana watu wa Aga Khan, ambapo tunaamini hatua hii itakwenda kuwasaidia watu wetu ambao wengi wao walikuwa wanashindwa kupata huduma za afya kutokana na changamoto za kipato.

“Kwahiyo kupitia makubaliano haya wanawake hawa watapatiwa bima ya afya ambayo gharama yake ni Sh 40,000 lakini wao watachangia Sh. 20,000 na iliyobaki itatolewa na wafadhili wengine. Na lengo letu ni kuhakikisha tunapata wafadhili wengine ili wakina mama hawa waweze kuchangia Sh. 10,000 tu…na bima hii itatumika katika vituo hivyo vilivyotajwa na kwa mwaka mzima,” amesema Lulu.

Naye mmoja wa wanawake hao wachuuzi, Aminata Rashid amesema: “Ninawashukuru sana Aga Khan kwa kuamua kutusaidia sisi wanawake, ilikuwa kwangu ni ndoto kama kuna siku nitamiliki bima ya afya na kutibiwa Hospitali kubwa kama za Aga Khan,”.