Na Esther Macha, Timesmajira Online, Ruvuma
TAASISI ya utafiti wa kilimo nchini (TARI)inatarajia kuanza kupima afya ya udongo ili kujua vitu vilivyopo ikiwemo rutuba na athari zitokanazo na matumizi ya pembejeo na pia kutoa ushauri kwa wakulima ili waweze kuzalisha kwa tija.
Hayo yamesemwa juzi na Mkurugenzi taasisi ya utafiti na kilimo nchini (TARI)Kituo cha Uyole, Dkt. Tulole Bucheyeki wakati wa kuzindua mradi huo na kusema kuwa maeneo yatakayonufaika na mradi huo ni kupima udongo kwenye mashamba ya wakulima na kutoa ushauri wa kitalaam namna bora ya kuzalisha mazao yao.
Aidha Mkurugenzi huyo amesema kuwa mradi huo wa kupima afya ya udongo utahusisha mikoa sita ikiwamo Ruvuma, Katavi, Kigoma, Arusha Manyara na Kilimanjaro kila mkoa utafanyiwa utafiti na majibu kutolewa na kupitia utafiti huo tutatoa ushauri wa kitalaam namna ya kukabiliana na athari zilizopatikana kwenye udongo.
Akizindua mradi huo, Mkuu wa Ruvuma, Brigedia Generali Wilbert Ibuge , amesema mpango huu wa tathmini ya utafiti wa udongo kwa mkoa wa Ruvuma utasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali yakiwamo ya chakula na biashara na kuufanya mkoa huo kuwa kinara wa uzalishaji wa mazao nchini.
“Mradi huu umekuja muda mwafaka hivyo tunaamini kuwa wakulima wa mkoa wa Ruvuma watanufaika na upimaji wa udongo ambao utakuwa na Afya ambapo matokeo yake mkulima ataweza kuzalisha mazao mengi ya biashara”alisema Mkuu huyo wa mkoa.
Mkurugenzi wa Kampuni ya OCP Tanzania, Dkt. Mshindo Msolla, ameleeza kuwa malengo ya mradi ni kutibu afya ya udongo ambayo kwa kiasi kikubwa nchini imeathirika na matumizi ya pembejeo zenye kemikali ambazo zimeathiri ardhi nyingi za kilimo.
Mtafiti wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo Tanzania Tari kutoka makao makuu Dodoma, Magreth Mchomvi alisema utafiti huo utasaidia kila mkulima kufahamu afya ya udongo na itamsaidia kupunguza gharama za ununuzi wa mbolea ambazo hazihitajiki katika ardhi yake.
Aidha Mchomvi amesema matokeo hayo ya utafiti yatamsaidia mkulima kutumia eneo dogo ya ardhi yake ambalo limekwisha fanyiwa utafiti kulima kwa ajili ya kuzalisha mazao mengi kwa ajili ya kukidhi mahitaji yake.
Mtafiti mwingine Fedrick Mlowe amesema zoezi hilo litahusisha wananchi, wataalamu kutoka kila Halmashauri za mikoa hiyo na vijiji 100 kila mkoa vitanufaika na zoezi hilo la upimaji.
Mlowe amesema ushirikishwaji wa wakulima kati zaezi hilo ni muhimu kutokana na wao kuendelea kufanyazoezi hilo la utambuzi wa afya ya udongo ambapo itasaidia kuwasaidia wakulima wengine namna ya kutambua afya ya udongo katika mashamba yao.
Hamis Haule ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, amesema ni fursa kwao kwani watapata majibu ya afya ya udongo na kushauriwa ni kwa namna gani wataweza kuzalisha kwa tija na kujikwamua na umasikini kupitia shughuli za kilimo.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba