December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Taasisi ya Nelson Mandela kuingiza Sokoni Mfumo wa kubaini machapishoya wizi

Na Doreen Aloyce, TimesMajira Online, Dodoma

TAASISI ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela imesema ipo mbioni kuingiza sokoni mfumo maalumu wa kubaini machapisho ya wizi.

Pia katika Kuendeleza Sayansi, Teknolojia na Ubunifu hapa nchini kupitia tafiti mbalimbali mpaka sasa taasisi hiyo imefanikiwa kufanya bunifu 73 ambazo ni matokeo ya ushirikiano kati ya wahadhiri na wanafunzi pamoja na Serikali na wadau wa maendeleo kutoka nje ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 20,2022 jijini Dodoma kuhusu shughuli za taasisi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa Mwaka wa Fedha 2022/23 Makamu Mkuu wa Chuo, Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Prof. Emmanuel Luoga amesema kuwa Taasisi hiyo imejikita katika matumizi ya TEHAMA ambapo itapata Dola za Marekani milioni 10 mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia, fedha hiyo itatumika kuimarisha mifumo ya TEHAMA na kuhakikisha inapata ithibati ya maabara ya viwango vya kimataifa.

” Ili kuwa na taifa linalojitegemea katika masuala ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ni lazima kuboresha eneo la tafiti ambapo kwa sasa Taasisi hiyo inaendelea na tafiti mbalimbali ikiwemo kuzalisha viuatilifu asilia ili kupambana na magonjwa ya mimea, hivyo kuongeza tija katika kilimo,”.

Na kuongeza”Katika masuala ya utafiti na ubunifu, mpaka sasa taasisi yetu imefanikiwa kufanya bunifu 73 ambazo ni matokeo ya ushirikiano wa hali ya juu kati ya wahadhiri na wanafunzi pamoja na Serikali na wadau wa maendeleo kutoka nje ya nchi,”Amesema Prof.Luoga

Pia amesema Taasisi yao kwa kushirikiana na taasisi zingine mbili zinaazisha Kituo cha Umahiri cha Ndizi ambacho kitahusika na masuala ya utafiti wa mbegu, namna ya kuongeza tija katika upandaji na usimamizi wa zao la ndizi na matumizi bor

Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23, Serikali imeidhinisha bajeti ya takriban Shilingi bilioni 43 kwa ajili ya taasisi hiyo ambapo Prof.Luoga amebainisha kuwa moja ya kipaumbele kikubwa ni ujenzi wa bweni maalum kwa ajili ya wanachuo wanawake wenye mahitaji maalum na wenye watoto wadogo ambao mradi huo tayari umeshaanza tangu Oktoba, 2021 na kiasi cha Shilingi bilioni 1.7 kimeshatumika.

“Ujenzi huu utafanyika kwa awamu tatu, awamu ya kwanza ambayo itachukua wanafunzi 180 imekadiriwa kutumia Shilingi bilioni 4.8 na inatarajiwa kukamilika Juni, 2023. Ujenzi wake umefikia asilimia 43,”Amesema Prof.Luoga

Prof.Luoga amesema kuwa mnamo Mwaka 2021, taasisi ilitengeneza Mpango Mkakati mpya ambapo chuo kimejitanua kwa kuongeza ngazi mbili za masuala ya atamizi za teknolojia na ubiasharishaji.

“Kuelekea miaka 61 ya Uhuru, Taasisi imejikita katika kufahamika na kufahamu filosofia ya chuo kutoka hatua tatu za kufundisha, kufanya utafiti na uenezi kwenda kwenye hatua tano kwa kuongeza masuala ya uatamizi na ubiasharishaji,”Amebainisha Prof.Luoga

Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa idara ya Habari Maelezo Gerson Msigwa amesema kuwa mbalimbali,Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela ni cha kitaaluma na mwelekeo wake ni kufanya kazi ya kuunganisha kati ya wanataaluma na jamii ndio maana kimejikita zaidi katika tafiti, hili ni eneo muhimu ambalo nchi inalihitaji.

“Serikali inatambua kwamba bila sayansi hakuna maendeleo, mageuzi wala mapinduzi yoyote ya kiuchumi, hivyo tunataka tutumie sayansi kama moja ya nguzo zitakazotuvusha kwenda kwenye maendeleo zaidi,”amesema Msigwa.