April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Taasisi ya AMEND, Ubalozi wa Uswiss yawanoa bodaboda mkoani Tanga

Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraOnline, Tanga

TAASISI ya AMEND kwa kushirikiana na Ubalozi wa Uswiss nchini Tanzania wametoa elimu ya huduma ya kwanza kwa madereva bodaboda wa Jiji la Tanga, ambako mradi wa elimu ya Usalama Barabarani inaendelea kutolewa kwa madereva hao.

Mafunzo hayo ya huduma ya kwanza kwa madereva wa bodaboda yanakwenda sambamba na elimu ya Usalama Barabarani inayotolewa na Taasisi ya AMEND kwa kushirikiana na Ubalozi wa Uswiss, ambao ndio wanaofadhili mradi wa utoaji mafunzo hayo kwa madereva bodaboda.

Akieleza zaidi kuhusu mafunzo hayo CPL Hamisi anayetoka Kitengo cha Elimu Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga amesema wanaushukuru AMEND na Ubalozi wa Uswisi kwa kuona haja ya kutekeleza mradi huo kwani unakwenda kuongeza uelewa kwa madereva bodaboda kujiepusha na ajali pamoja na kutoa huduma ya kwanza inapotokea ajali.

“Ni muhimu kutolewa kwa huduma ya kwanza pale ajali inapotokea, huku akisisitiza anapaswa kutoa hiyo ni mtu aliyepata elimu ya mafunzo ya jinsi ya kutoa huduma ya kwanza kwa mtu aliyepata ajali.

Mafunzo haya yatasaidia kuokoa maisha kwa mtu aliyepata ajali ya bodaboda,”amesema.

Ametoa mwito kwa baadhi ya bodaboda kuacha kujihusisha na vitendo vya uhalifu zinapotokea ajali na badala yake watumie elimu waliyoipata kuokoa maisha ya waliopatwa na ajali barabarani.

Wakati huo huo, Diana Kashmiry kutoka Kikosi kazi cha huduma ya kwanza- Shirika la Msalaba Mwekundu alisema elimu wanayoitoa inamuwezesha dereva bodaboda kufahamu changamoto aliyoipata mtu ajalini na jinsi ya kumsaidia kwa kumpa huduma ya kwanza

Aidha, ametoa angalizo kutokana na mazingira hatarishi yanayokuwepo katika ajali, ni vema kwa mtu asiye na vifaa vya kutoa huduma ya kwanza asiye huduma hiyo ili kumuepusha na madhara yanayoweza kujitokeza yakiwemo ya magonjwa ya kuambukiza.

Kwa upande wake Ofisa Miradi kutoka AMEND Scolastica Mbilinyi alieleza kwamba lengo la kutoa elimu ya huduma ya kwanza kwa bodaboda ni kusaidia kuokoa maisha ya watu pindi ajali zinapotokea.

Ameongeza kwamba wamekuwa na mradi huo wa kutoa mafunzo ya usalama barabarani kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Jeshi la Polisi na Msalaba Mwekundu pamoja na wadau wote muhimu.

Aidha amesema AMEND miongoni mwa mambo wanayofanya ni pamoja na kutoa elimu ya usalama barabarani, ujenzi wa miundombinu ya barabara kwenye shule zilizopo maeneo hatarishi na kwa wakati huu huo wanatoa mafunzo ya huduma ya kwanza kwa madereva.

Pamoja na hayo amesema mpaka sasa AMEND kwa ufadhili wa ubalozi wa Uswiswi wameshatoa elimu ya usalama barabarani katika mikoa ya Tanga na Dodoma na lengo ni kuwafikia madereva wa bodaboda 750, huku akisisitiza kwa Mkoa wa Tanga wanatarajia kutoa elimu hiyo katika Wilaya zote za Mkoa huo.