April 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Taarifa za maendeleo ziwafikie wananchi kwa usahihi

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira

Makamu wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema kuelekea uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka 2025, wananchi wanapaswa kupewa taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu miradi mbalimbali ya maendeleo iliyofanywa na Serikali zote mbili ili waweze kufanya tathmini na maamuzi wakati wa Uchaguzi wa viongozi wao.

Abdullah ameyasema hayo leo wakati akifungua Kikao kazi cha 20 cha Maafisa Habari wa Serikali kinachofanyika katika ukumbi wa New Aman Complex, Zanzibar.

Abdulla amesema miongoni mwa miradi inayotekelezwa na Serikali ya Muungano ni ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR ili kuimarisha huduma za usafiri wa haraka na kuleta Mapinduzi ya huduma za usafirishaji wa abiria na mizigo hapa nchini, ujenzi wa viwanja vya mpira na mradi wa umeme wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere ili kuwafikishia wananchi huduma ya umeme.

Aidha, amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kuimarisha Uwanja cha Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume na vilevile kuanza ujenzi wa uwanja mpya wa ndege wa kimataifa kisiwani Pemba.

Miradi mingine ya maendeleo inayotekelezwa ni pamoja na uboreshaji wa Bandari ya Malindi, Bandari ya Mkoani, Bandari ya Wete, Bandari ya Mkokotoni, kuanza ujenzi wa Bandari Jumuishi ya Mangapawani, ujenzi wa Bandari ya Fumba ambayo imeanza kazi na ukamilishaji wa ujenzi wa Bandari ya Shumba Mjini.

Amesema kuwa miradi yote hii itakapokamilika inakusudiwa kurahisisha upatikanaji wa huduma, kut]rahisisha usafiri na usafirishaji wa mizigo na kupunguza gharama za upatikanaji wa bidhaa kwa wananchi pia kuchochea harakati za kiuchumi hapa nchini huku akisisitiza kuwa miradi hiyo ni kielelezo cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii yaliyopigwa na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Ni wazi kada yenu ina mchango mkubwa kwenye kuhabarisha umma, lakini bado mna kazi kubwa ya kuongeza juhudi ya kuhabarisha Umma kuhusu miradi yote ya maendeleo ili waweze kufanya maamuzi sahihi,”amesema Abdullah.

Pamoja na mambo mengine, Abdullah amewataka maafisa hao waongeze juhudi katika kuhanbarisha umma kwa kutoa taarifa sahihi za miradi mbalimbali ya Serikali akibainisha kuwa Serikali zote mbili zitaendelea kuimarisha demokrasia, utawala bora na haki za binadamu sambamba na kuweka nguvu kwenye mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi na udhalilishaji wa aina zote.