Na Iddy Lugendo, Timesmajiea Online DSM
SWAHILI Fashion Week & Awards 2024 inatarajiwa kuwakutanisha wabunifu 40 kutoka nchi takribani nne kwa lengo la kutangaza matumizi ya nishati safi na kutambua umuhimu wa kukuza ubunifu unaozingatia uendelevu wa mazingira na kujenga ajira barani Afrika.
Jukwaa hilo likiwa ni msimu wake wa 17 na litakalofanyika kuanzia Desemba 6 hadi 8, 2024 katika Ukumbi wa Parthenon Hall, Dar es Salaam, lenye ya kaulimbiu isemayo “Discover what makes Africa beautiful.”
Akizungumza jijini Dar es salaam Balozi wa Italia nchini Tanzania, Giuseppe Sean Coppola, amesema Swahili Fashion Week ni jukwaa muhimu linaloshirikisha wabunifu kutoka pande mbalimbali za dunia, huku likiimarisha ushirikiano wa kiutamaduni na kiuchumi kati ya Tanzania na Italia.
“Swahili Fashion Week inatoa nafasi kwa wabunifu kuonyesha kazi zao, kukuza ajira, na kuchangia maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,” amesema Balozi Coppola.
Kaimu Mkurugenzi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Edward Buganga, amesisitiza kuwa tukio hili lina mchango mkubwa katika kukuza tamaduni za Kiswahili na kuimarisha uchumi wa taifa. “Swahili Fashion Week ni zaidi ya maonyesho ya mitindo; ni jukwaa linalochangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha sekta ya sanaa na kuongeza ajira kwa vijana”.
Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Swahili Fashion Week, Mustafa Hassanali, ameongeza kuwa tukio hili linatoa fursa kwa wabunifu na wanamitindo kujionyesha kimataifa. “Ni wakati wa kuthubutu na kuchangamkia fursa hii ya kujenga majina na kufanikiwa katika sekta ya mitindo”.
Kwa kushirikiana na Ubalozi wa Italia na Camera Nazionale della Moda Italiana, wabunifu kutoka Italia, Uganda, Kenya na Tanzania wataungana kuonyesha ubunifu wao na tukio hilo pia litatambua vipaji bora kwa kutoa tuzo 27 kwa washindi, ikiwa ni sehemu ya kuenzi ubora katika tasnia ya mitindo.
More Stories
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam
MSF ilivyojidhatiti kusaidia serikali katika utoaji wa huduma za afya
Prof.Muhongo awapongeza vijana 32 waliotembea kwa miguu kutoka Butiama hadi Mwanza