Na Mwandishi Maalum
SUMUKUVU (mycotoxins) ni sumu zinazozalishwa na kuvu/fangasi (fungus) wa makundi mbalimbali) wanaoota zaidi kwenye mazao ya chakula kama vile mahindi na karanga. Sumukuvu huweza kuzalishwa kwenye mazao yakiwa katika hatua mbalimbali kama vile:
• shambani,
• baada ya kuvunwa
• wakati wa kusafirisha au
• kuhifadhi
Kumbuka: Sumukuvu zinapokuwepo kwenye mazao au bidhaa huendelea kubaki hata baada ya chakula kupikwa au kusindikwa.
Aina ya kuvu wanaosababisa sumukuvu
Kuna aina nyingi za kuvu wanaoweza kushambulia mazao. Aidha kuvu wa makundi matatu yaani Aspergillus, Penicillium na Fusarium ndio hasa wanahusika na kuzalisha sumukuvu kwenye mazao ya nafaka na mbegu za mafuta.
Aina za sumukuvu
Zipo aina nyingi za sumukuvu ambazo huzalishwa na kuvu tofauti. Kwa kulinganisha kiwango cha uchafuzi wa sumukuvu katika mazao ya chakula pamoja na kiwango cha madhara ya kiafya kwa binadamu yatokanayo na sumukuvu, kwa hapa Tanzania sumukuvu aina ya aflatoxins na fumonisins ndiyo tatizo zaidi.
Kumbuka: Uwepo wa kuvu na kuzalisha sumukuvu unategemea na hali ya hewa ya mahali husika, hivyo maeneo tufauti huweza kuwa na kiwango na aina tofauti za kuvu.
Dalili za uchafuzi wa sumukuvu kwenye mazao ya chakula
Sumukuvu zinapokuwepo kwenye mazao au bidhaa, hazionekani kwa macho. Pia huendelea kubaki hata baada ya chakula kupikwa au kusindikwa. Dalili ya mazao yaliyochafuliwa na sumukuvu ni pamoja na:
• Ukungu/kuvu
• Harufu ya uvundo
• Nafaka kutengeneza vumbi
• Nafaka kugandamana
• Nafaka kubadilika rangi, kuwa na weusi
Mahindi na karanga ni mojawapo ya mazao muhimu ya chakula ambayo hushambuliwa na fangasi wanaozalisha sumukuvu kwa wingi
Mazao yaliyoshambuliwa na kuvu
Sumukuvu inavyoweza kumfikia mlaji
Mlaji huweza kupata sumukuvu endapo:
• Atakula chakula kilichochafuliwa na sumu hiyo.
• Atakula mazao yanayotokana na mifugo kama vile maziwa endapo mifugo italishwa chakula kilichochafuliwa na sumukuvu. (Mfano mashudu ama nafaka mbovu).
• Mtoto atanyonya maziwa ya mama aliyekula chakula kilichochafuliwa na sumukuvu.
Madhara yatokanayo na sumukuvu
Madhara ya kiafya
Ulaji wa vyakula vilivyochafuliwa na sumukuvu huweza kusababisha madhara mbalimbali ya kiafya. Madhara hayo huweza kujitokeza ndani ya muda mfupi au baada ya muda mrefu kutegemeana na; kiasi cha sumukuvu kilichopo kwenye chakula kilicholiwa, kiasi cha chakula na idadi ya milo ya chakula kilichochafuliwa, pamoja na umri na hali ya afya ya mlaji.
Madhara yanayotokea ndani ya muda mfupi
Madhara ya sumukuvu kiafya ambayo huweza kutokea ndani ya muda mfupi husababishwa na ulaji wa kiasi kikubwa cha sumukuvu. Madhara hayo ni pamoja na kuathirika kwa ini, figo, mfumo wa fahamu pamoja na kupunguza uwezo wa damu kuganda na hata kifo.
Athari za sumukuvu kiuchumi
Katika biashara za ndani, kikanda na kimataifa, uchafuzi wa sumukuvu husababisha athari zifuatazo;
i. Kukataliwa kwa bidhaa za chakula zilizozidi viwango vya sumukuvu vinavyokubalika katika soko na hivyo kukosa mapato.
ii. Kupungua kwa akiba ya chakula, (chakula kilichochafuliwa zaidi ya kiwango kinachoruhusiwa, hakifai kwa matumizi ya binadamu na mifugo hivyo hutakiwa kuharibiwa).
iii. Kuongezeka kwa gharama za matibabu
iv. Kupungua kwa nguvu kazi na uzalishaji mali.
Jinsi ya kudhibiti sumukuvu
Kumbuka:
• Wadudu wasipodhibitiwa huongeza unyevu na joto katika ghala ambavyo huchochea kuvu kuzaliana na kuzalisha sumukuvu
• Viuatilifu visipotumiwa kwa usahihi vinaweza kuathiri afya ya mlaji. Hivyo zingatia matumizi ya viuatilifu kwa kiwango sahihi na muda ambao mazao yaliyowekwa viuatilifu yanahifadhiwa kabla ya kuruhusiwa kwa matumizi.
Udhibiti wa sumukuvu wakati wa kuandaa mazao kwa ajili ya chakula
• Peta na chambua kuondoa taka, mbegu hafifu, zilizopasuka, zilizooza, zilizobadilika rangi na zilizoharibiwa na wadudu
• Osha kundoa vumbi, udongo na punje dhaifu
• Koboa mahindi kabla ya kusaga
• Baada ya kusaga mahindi, hifadhi unga kwenye chombo safi kisichoruhusu unyevu
Kumbukuka: Kupungua kwa sumukuvu kwa njia ya kukoboa hutegemea na kiwango cha punje za mazao zilizoharibika au kuoza.
More Stories
Madaktari bingwa wa Samia watua Rukwa
Utashi wa Rais Samia na matokeo ya kujivunia vita dawa za kulevya nchini
Uwekezaji wa Rais Samia sekta ya afya waendelea kuwa lulu Afrika