Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
WAKALA ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) imesema katika mwaka ujao wa fedha 2022/2023 inatarajia kuongeza wigo wa kufanya vipimo vya ubora wa vyakula vya mifugo ili kubaini aina za sumu kuvu ambazo zinaweza kusababisha madhara ya kiafya kwa binadamu na mifugo.
Mtendaji Mkuu wa TVLA Dkt. Stella Bitanyi alibainisha hayo ofisini kwake jijini Dar es Salaam, wakati wa zoezi la kuhakiki ubora wa vyakula vya mifugo vinavyozalishwa hapa nchini lililofanyika mwishoni mwa wiki, zoezi ambalo limefanywa katika wilaya za Temeke na Ubungo na wataalamu kutoka TVLA.
Dkt. Bitanyi alisema wakala hiyo inatarajia pia kupima mabaki ya ‘antibiotic’ na dawa nyingine za mifugo ndani ya vyakula vya mifugo ili kuhakikisha ubora wa vyakula vya mifugo kwa kutokuwa na mabaki ya dawa ambazo zinaweza kusababisha usugu wa dawa kwa mifugo pamoja na binadamu atakayetumia mazao yanayotokana na mifugo hiyo.
Katika hatua nyingine mtendaji mkuu huyo wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), alitoa wito kwa wazalishaji wa vyakula vya mifugo nchini pamoja na wafugaji kuhakikisha wanafikisha sampuli za vyakula katika maabara hiyo ili kupima ubora wa chakula ambacho kinastahili kutumiwa na mifugo pamoja na malighafi ambazo zitatumiwa katika kutengeneza vyakula hivyo.
Alibainisha kuwa matumizi ya vyakula sahihi vya mifugo ambavyo vina virutubisho vinavyostahili, vitamuwezesha mfugaji kufuga kwa tija kwa kuwa mifugo itakuwa katika muda unaotakiwa kitaalamu na kufikia kiwango cha uzito unaotakiwa sokoni.
Akizungumza wakati wa zoezi la kukagua ubora wa vyakula vya mifugo katika Wilaya za Temeke na Ubungo,Afisa Mtafiti wa Mifugo kutoka TVLA Dkt. Evaline Mfuru alisema uwiano sawa wa virutubisho vinavyotakiwa kwenye vyakula vya mifugo kwa kiasi kikubwa hupunguza gharama za uzalishaji pamoja na kudhibiti magonjwa ya mifugo.
Nao baadhi ya wafugaji na wazalishaji wa vyakula vya mifugo wamesema zoezi la uhakiki wa ubora wa vyakula vya mifugo litakuwa na tija kwa kuhakikisha vinapatikana vyakula bora, ambavyo vitaleta tija kwa mfugaji pamoja na kuondoa sokoni vyakula vya mifugo ambavyo havikidhi vigezo.
Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) ambayo iko chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikifanya uchunguzi wa ubora wa vyakula vya mifugo ili vyakula hivyo viwe katika viwango vinavyotakiwa kwa ajili ya matumizi ya mifugo na kuleta tija kwa mfugaji.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba