May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

SUMAJKT kujenga nyumba za waathirika wa maporomoko ya udongo Hanang

Na Mwandishi wetu ,Manyara

HALMASHAURI ya Hanang’ imetiliana saini na Shirika la uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT) kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 108 za waathirika wa maporomoko ya udongo yaliyotokea hivi karibuni Katesh katika wilaya ya Hanang mkoani Manyara.

Mkuu wa  mkoa wa Manyara Queen Sendiga ameshuhudia utiaji saini huo ambapo amesema kutokana na kazi ambazo zimekuwa zikifanywa na SUMAJKT ana mategemeo makubwa kuwa watajenga  nyumba  zilizo bora na kukamilika kwa wakati.

“Tunategemea na kwa uzoefu wao SUMAJKT ambao wao wenyewe wamekiri kwamba nyumba hizi zitajengwa katika mtindo wa oparesheni hivyo zitajengwa kwa muda mfupi ,na hata mimi nakiri kwamba zitamalizika katika muda mfupi na kwa ubora unaotakiwa na watakaopata nyumba hizo wajue kweli wamepata nyumba.”amesema

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa SUMAJKT Kanali Petro Ngata,  ameeleza kuwa SUMAJKT ipo tayari kutekeleza jukumu ililopewa na serikali na katika muda waliopangiwa kutekeleza na kwamba watakamilisha jukumu hilo wa wakati.

Mshauri wa ujenzi huo kutoka ofisi ya Waziri Mkuu Joseph Msangi, amesema kuwa maandalizi ya ujenzi wa nyumba hizo tayari yamekamilika.

Amesema SUMAJKT limekuwa likipatiwa miradi ya kimkakati na serikali kutokana na utendaji wa kazi kwa ufanisi, ubora na kumaliza kazi kwa wakati.