November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sukari ipo ya kutosha

Na Martha Fatael, TimesMajira Online, Moshi

MENEJIMENTI ya Kiwanda cha Sukari (TPC) wilayani Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro, imeihakikishia serikali na wananchi kuwa pamoja na kwamba inaelekea kufunga msimu wa uzalishaji, bado sukari itakuwepo sokoni.

Akizungumza mbele ya Waziri wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda, Afisa Mtendaji na Utawala wa kiwanda hicho, Jafaary Ally amesema kiwanda kimezalisha sukari ya kutosha kwa muda wote ambao kiwanda kitakuwa kimefungwa.

Kauli hiyo inafuatia mfumo wa mazoea unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu ili kuficha bidhaa hiyo na kusingizia uhaba wa bidhaa hiyo kwaajili ya kuongeza bei ya sukari sokoni.

Ally anasema mwaka huu wamezalisha tani 103,000 na kupita malengo ya msimu uliopita wa kuzalisha tani 95,000 ambao ulidhiriwa na mafuriko hivyo kuathiri miwa sanjari na kuwa na ugonjwa wa Miwa (Yellow sugar cane).

“TPC iwatoe hofu wananchi, sukari itakuwepo ya kutosha na ikitokea kuna upungufu, basi serikali imejipanga kuhakikisha inakabili upungufu huo hususan kipindi cha May na Juni ambapo tutakuwa bado tumefunga kiwanda” amesema Ally.

Akizungumza na uongozi wa kiwanda hicho pamoja na baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya Sukari nchini, Waziri Mkenda amesema serikali itaendelea kuvilinda viwanda vya ndani ili kuhakikisha haviathiriwi na sukari ya magendo.

“Kwa muda fulani uwekezaji uliathiriwa na uingizwaji wa sukari kutoka nje….lakini kwa miaka mitano iliyopita serikali imedhibiti uingizwaji wa sukari, hivyo viwanda vya ndani kutoathiriwa na sukari ya magendo” amesema.