July 4, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

STAMICO yaja na mkaa mbadala maonesho sabasaba

Joyce Kasiki,Timesmajira online

WAKATI Rais Samia Suluhu Hassan akiendelea kusisitiza kuhusu matumizi ya Nishati safi ya kupikia kwa ajili ya utunzaji wa mazingira,Shirika la Madini (STAMICO) limekuja na nishati mbadala ya mkaa wa mawe ili kuelimisha wananchi.

STAMICO ni moja ya taasisi zinazoshiriki maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) ambalo limekuja na mkaa mbadala aina ya RAFIKI BRIQUETTES unaodumu zaidi ,rafiki kwa matumizi,rafiki kwa mazingira na bei nafuu kwa mtumiaji hadi wa hali ya chini.

Hii ni kutokana na mabadiliko ya tabianchi ambayo imesababishwa na uharibifu wa mazingira kutokana na ukataji wa miti kwa ajili ya kupata nishati ya kupikia ya kuni na mkaa.

Katika siku za hivi karibuni,viongozi mbalimbali akiwemo Rais Dkt.Samia na viongozi walio chini yake wamekuwa wakisisitiza matumizi ya nishati mbadala ambapo katika maonesho ya wiki ya Nishati Bungeni jijini Dodoma Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwahimiza wananchi kuanza kubadili matumizi ya nishati ya kuni na mkaa na kwenda kwenye nishati safi ya kupikia.

Aidha alizitaka taasisi zinaohudumia watu zaidi 100 kuhakikisha mpaka Disemba mwaka huu ziwe zimeachana na matumizi ya kuni na mkaa ili kuokoa mazingira.