December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Spika Dkt. Tulia asitisha agizo la kuwaondoa wakulima

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

SPIKA wa Bunge na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Dkt Tulia Ackson amesitisha agizo la Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dkt Rashid Chuachua la kuwataka kuondoka wakulima 1,700 wa skimu ya umwagiliaji katika Bonde la uyole Jijini Mbeya.

Dkt, Tulia amefikia hatua hiyo leo siku mbili baada ya Mkuu huyo wa Wilaya ya kufanya mkutano wa hadhara wa wananchi na wakulima wa bonde hilo Julai 19 mwaka huu jambo ambao wananchi hawakukubaliana nalo na kulipinga

”Nimeshtushwa sana baada ya kupata taarifa nimefika hapa nasema hamuondoki endeleeni na shughuli za uzalishaji kwani bonde hilo hata kabla sisi hatujazaliwa wazee wetu walikuwa wakilitumia kuzalisha mazao ya chakula na biashara,” amesema.

Dkt, Tulia amesema kuwa amefikia maagizo hayo ya Serikali amelazimika kukutana na panda zote mbili kuzungumza nao na kupata taarifa za eneo hilo na ndio sababu ya kusitisha huku uongozi wa wakulima kuendelea na taratabu za kubadilisha hati.

”Wananchi nyie sio wavamizi niwatoe hofu kwani hapo awali wanaosema hili eneo ni la Wizara ya Afya walikuwa wapi! nasema hapa hamtaondoka na Mstahiki Meya, Dourmohamed Issa amenihakikishia Jiji wafatenga eneo jingine kwa ajili ya uwezeshaji wa huduma za afya na mgogoro huu umekwisha ” amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dkt.Rashid Chuachua amesema kuwa mkutano huo ni Spika hivyo wanahitaji busara zake kutatua mgogoro huo.

Aidha Mwanasheria wa Bonde hilo, Shambwee Shitambala amesema agiz alilolitoa Mkuu wa Wilaya kwenye mkutano wa Hadhara Julai 19 halikukubaliwa na wananchi wa eneo hilo.

“Agizo hilo wananchi walilingana nalo na mimi kama Mwanasheria wao nilifanya taratabu zote za kisheria kutokana na eneo hilo kuwa la asili tangu enzi za mababu na halina maeneo ya mipaka inayoonyesha kuwa ni mali ya wizara ya Afya” amesema Shitambala.

Makamu Mwenyekiti wa wakulima wa Bonde hilo, Hezron Mwakingili amesema kuwa eneo hilo lina ukubwa wa hekta 120 ambazo zinazalisha mazao mbali mbali ya chakula na biashara. Mwisho.