* Ni dhidi ya janga la Corona, watakiwa kupunguza safari za Dar, mizunguko ya Dodoma, awaelekeza mtindo mpya wa kuishi kipindi hiki
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, ametoa mwongozo wenye vipengele vinne kuhusu tahadhari ya kujikinga na maambukizo ya ugonjwa wa Corona kwa wabunge ikiwemo kutakiwa kupunguza safari za Dar es Salaam.
Mwongozo huo ulisomwa juzi Bungeni jijini Dodoma na Naibu Spika, Dkt. Tulia Ackson. Alisema tangu kutangazwa kwa ugonjwa wa Corona hapa nchini Machi 16, 2020 hatua mbalimbali za kitaifa zimechukuliwa kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa huo.
Hata hivyo, alisema kwa kuzingatia ongezeko la maambukizi ya ugonjwa huo hapa nchini, wao kama Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanao wajibu wa kuchukua tahadhari zaidi ya ugonjwa wa corona ili kukamilisha jukumu lililo mbele yao kwa sasa la kupitisha bajeti ya Serikali 2020/21 na kutunga sheria mbalimbali.
Dkt. Tulia alisema kwa sababu hiyo Spika amepeleka kwao mwongozo wa kukabiliana na ugonjwa wa Corona wenye vipengele vinne.
Moja, Dkt. Tulia alisema taarifa ya Waziri wa Afya ya Aprili 15, mwaka huu imeonekana kuongezeka maambukizi katika Jiji la Dar es Salaam na Zanzibar na maambukizi mapya katika maeneo ya Arusha, Kilimanjaro, Mwanza na Kagera.
Kutokana na ongezeko hilo, Dkt. Tulia alisema ni muhimu sana kupunguza safari za Dar es Salaam na maeneo mengine kwa ujumla ikiwemo Dodoma na hiyo itasaidia kupunguza hatari ya maambukizi katika nchi yetu.
Pili, kupitia mwongozi huo Spika aliwataka wabunge kuzingatia umbali kati ya mtu na mtu na punguza mizunguko ndani ya jiji la Dodoma. “Mheshimiwa Spika anawashauri na kuwasisitiza kwamba mtindo wa nyumbani-bungeni-nyumbani iwe ndiyo mwenendo wa maisha kwa wakati huu na hata mahitaji ya nyumbani kutoka sokoni kuwe na siku maalum ikiwezekana mara moja kwa wiki,” alisema Naibu Spika wakati akisoma mwongozo huo.
Tatu, Naibu Spika alisema kulingana na taarifa za wataalam wa afya ugonjwa wa corona umeonekana kuwa madhara zaidi kwa wazee na watu wenye magonjwa sugu, kama kisukari, shinikizo la moyo, pumu, kifua kikuu, saratani,figo na mengine, hivyo ni vema zaidi wenye maradhi hayo wakachukua tahadhari zaidi ya kujikinga na ugonjwa huo.
Aliwataka wabunge kuendelea kufuata ushauri wa kunawa mara kwa mara kwa maji na sabuni pamoja na matumizi ya vitakasa mikono ili kuendelea kujikinga na maambukizi ya virusi hivyo. “Pamoja na hayo yote ni muhimu kuzingatia lishe bora, maji ya kunywa ya kutosha, mazoezi na kupata muda wa kupumzika kwani hayo ni mambo muhimu katika kuimarisha afya zetu,” alisema na kuwataka wabunge
kuepuka kufuatilia habari za kuogopesha na kujenga hofu, kwani hofu inaweza kuongeza msongo wa mawazo na kuzoretesha afya zetu.
Alisema mwongozo huo umetumwa kwa wabunge wote hivyo wanatakiwa kuyatilia maanani na wale wenye maradhi yaliyotajwa ni muhimu Zaidi kufuatilia afya zao katika kipindi hiki, lakini kukaa mbali na watu ambao wanaweza kutuletea madhara
More Stories
Mhandisi Samamba awasisitiza maafisa madini kusimamia usalama wa migoni msimu wa mvua
Wapinzani kutimkia CCM ishara ya ushindi Uchaguzi Serikali za Mitaa
Vikundi Ileje vyakabidhiwa mikopo ya asilimia 10, DC Mgomi avipa somo