May 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Asilimia 95 ya wagonjwa Corona waendekea vizuri

Na Penina Malundo

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amesema asilimia 95 ya wagonjwa waliopata maambukizi ya ugonjwa wa corona wanaendelea vizuri, isipokuwa wagonjwa wanne ndio wapo kwenye uangalizi maalum.

Wagonjwa hao wamelazwa katika vituo mbalimbali vya afya nchini. Akizungumza jijini Dar es Salaam jana wakati wa uzinduzi wa miongozo ya mpango wa Huduma za Afya katika Jamii na Matumizi ya Dashibodi ya Viashiria vya Elimu ya Afya kwa Umma, Waziri Ummy alisema taarifa aliyopata kutoka katika vituo vinavyopokea wagonjwa wa Corona nchini zinasema wanaendelea vizuri, isipokuwa hao wanne.

Alisema tangu kuanza kwa ugonjwa wa Corona nchini kwa kiasi kikubwa kumekuwa na mafanikio ya kubadilisha tabia na hulka za Watanzania kuhusu kunawa mikono. “Nafarijika sana kama Waziri wa Afya nikipita katika nyumba na kuona nje kuna ndoo na sabuni. Corona imekuja ila inatusaidia kuimarisha huduma ya kinga na kujiweka katika nafasi muhimu za kupambana na magonjwa yanayosababishwa na usafi,” alisema na kuongeza;

“Serikali imefanya tathmini na kupitia upya mfumo mzima wa utoaji wa huduma za afya katika jamii. Kupitia wahudumu wa afya ngazi ya jamii na tumegundua kwamba katika mwongozo wa huduma za afya ngazi ya jamii wa mwaka 2014 ulikuwa na mapungufu hivyo mwongozo huu umekuja na mabadiliko kadhaa ikiwemo idadi ya wahudumu wa afya ngazi ya kijiji kuongezeka na sio kuwa wawili kama mwanzo ,” alisema Ummy

Alisema kupitia miongozo hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kuwasaidia wahudumu wa afya hao kupewa elimu na kuhakikisha wananchi wanapata elimu kwa wakati hususani katika kipindi hiki cha ugonjwa wa Corona.

“Serikali itawatumia wahudumu hawa kuendelea kutoa elimu juu ya mambo ambayo wananchi wanatakiwa kuyafanya ili kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19. Wahudumu watajengewa uwezo na kupatiwa vitendea kazi kwa ajili ya kwenda kuanza kazi hii muhimu,” alisema na kuongeza

“Katika kupambana na mlipuko kama magonjwa ya Ebola na Covid-19 yanaweza kupunguzwa kwa kiasi kikubwa sana endapo tutaimarisha mifumo ya kutoa elimu na taarifa sahihi za kufuata kanuni za afya,” alisema Ummy

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Miradi ya USAID, Tulonge Afya,Waziri Nyoni aliipongeza Serikali kwa maamuzi ya kuufanya mfumo huo wa wahudumu wa afya wa jamii kwa kufanya uwe rasmi tofauti na awali. Alisema USAID imekuwa ikitumia mfumo wa wahudumu wa afya ya jamii katika kufanikisha miradi yake mingi ya afya nchini.