Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Mbeya.
Tangu kuanza kwa utaratibu wa kuwa na masoko ya madini, Mkoa wa Mbeya umepata mafanikio makubwa kupitia soko la madini la Chunya ambapo kwa sasa zinakusanywa Kilo 250 – 300 za dhahabu kwa mwezi ikilinganishwa na kilo 25 hapo awali kabla ya kuanzishwa kwa soko hilo mwaka 2018.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa wakati akifungua Maonesho ya Kwanza ya Teknolojia ya Madini yaliyofanyika katika viwanja vya Sinjiriri vilivyopo katika Mkoa wa Kimadini wa Chunya.
Katika hatua nyingine Dkt. Kiruswa amesema, Mapato ya Serikali katika mkoa wa Kimadini Chunya yameongezeka kutoka shilingi bilioni 5 hadi bilioni 30 kwa mwaka, leseni za madini zimeongezeka kutoka 150 mwaka 2018 hadi 1500 kwa sasa, leseni za uchenjuaji nazo zimeongezeka kutoka 4 mwaka 2018 hadi 250, leseni za biashara ndogo za madini (Brokers) kutoka 0 hadi 300 na leseni kubwa kutoka 0 hadi 60 kwa sasa.
Pamoja na mambo mengine, Dkt. Kiruswa amesema, Mchango wa Sekta ya madini umekuwa ukiimarika mwaka hadi mwaka ambapo mwaka 2017 Wizara ilipoanzishwa ulikua kutoka asilimia 4.4 mpaka asilimia 7.2 ya Pato la Taifa Mwaka 2021 aidha, katika robo tatu ya mwaka 2022 mchango umefikia asilimia 9.7 lengo la sekta ya Madini ni kuchangia asilimia 10 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2025.
Katika kuimarisha biashara ya madini nchini Serikali imeanzisha jumla ya masoko ya madini 42 na vituo vya manunuzi madini 93 nchini kote ambapo uwepo wa masoko hayo kumepunguza biashara ya utoroshaji wa madini kwa kuwa serikali imeboresha mazingira ya biashara ya madini.
Pia, Dkt. Kiruswa amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Zuberi Homera kwa kubuni na kuanzisha maonesho hayo ambayo yanaenda sambamba na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kufungua nchi ambapo mkoa wa mbeya umefunguliwa kwa maonesho kwa maonesho mara ya kwanza hayo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Homera ameipongeza Wizara ya Madini kwa kuendelea kutatua changamoto mbalimbali mkoani humo ambapo kwa sasa mkoa huo unaendelea kuimarika katika ukusanyaji wa mapato yatokanayo na Sekta ya Madini.
“Napenda kuwashukuru nyote mliokuja kwenye maonesho haya ambapo ni imani yangu kuwa, kwa kiwango kikubwa, yatakidhi matarajio ya wadau mbalimbali na ninawashukuru sana wale mliochangia kwa hali na mali kufanikisha Maonesho haya,” amesema Homera.
Mkoa wa Mbeya ni miongoni mwa mikoa iliyobarikiwa kuwa na madini ya aina mbalimbali kitu ambacho kimeufanya mkoa huo kuwa na mikoa miwili ya Kimadini ikiwemo Mkoa wa Madini Chunya na Mkoa wa Madini Mbeya.
Kwa ujumla kila wilaya ina fursa za kipekee za uwepo wa madini mbalimbali ambayo yanaufanya mkoa kuwa miongoni mwa mikoa yenye neema ya kipekee ya madini kwa mfano mkoa una utajiri mkubwa wa madini ya dhahabu, fedha, shaba, risasi, chuma, madini ya ujenzi, manganese, chromium, chokaa, mabo, madini mkakati, gesi ya ukaa na makaa ya mawe.
More Stories
Dkt.Mathayo:Dkt.Samia,Dkt.Mwinyi wanastahili,ajivunia mafanikio jimboni
Jokate achangia milioni 3 mfuko wa bodaboda
Mhandisi Kundo agoma kuweka jiwe la msingi mradi wa maji