Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline
JANUARI 12, Wazanzibar wataadhimisha miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Mapinduzi ya Zanzibar yalitokea mwaka 1964 ili kumuondoa madarakani Sultani wa Zanzibar na serikali yake, iliyoundwa hasa na Waarabu, na hatimaye kuweka uongozi mikononi mwa Waafrika.
Usultani wa Zanzibar ulikuwa umepewa na Uingereza uhuru wake mwaka 1963. Kabla ya hapo, Waarabu walikuwa wamefaulu kudumisha katika mfululizo wa chaguzi utawala waliokuwa nao tangu zamani za Zanzibar kuwa chini ya Usultani wa Omani.
Chama cha Afro-Shirazi Party (ASP), kilichowakilisha hasa Waafrika, kilipoona kwamba bungeni kina viti vichache ingawa kilipata asilimia 54 za kura katika uchaguzi wa Julai 1963, kilipatana na chama cha mrengo wa kushoto Umma Party.
Januari 12 , 1964 asubuhi na mapema, mwanachama wa ASP, John Okello kutoka Uganda aliongoza wanamapinduzi 600–800 wa kisiwa kikuu cha Unguja kushinda polisi wa nchi na kuteka silaha zao.
Halafu walielekea Zanzibar Town walipompindua, Sultani Jamshid bin Abdullah na serikali yake. Waliokufa katika mapigano wamekadiriwa kuwa 80 hivi tu.
Kiongozi wa ASP Abeid Karume, asiyekuwa na msimamo mkali akawa rais wa kwanza wa nchi, na wanachama wa Umma party walipewa nafasi Serikalini.
Mapinduzi ya Matukufu ya Zanzibar yalifanyika ili kuwaletea Wazazibar. Na hiyo inadhihirishwa na maendeleo yaliyopatikana visiwani humo katika kipindi chote cha awamu nane cha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Katika kuelekea Maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu, tumeshudia Rais Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akizindua miradi ya maendeleo.
Uzinduzi huo unadhihirisha kwamba lengo la Mapinduzi linaendelea kutimizwa na kilichobakia ni kuendelea pia kulinda Uhuru wa wananchi wa Zanzibar.
Katika mwendelezo wa kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar, tumeshuhudia uwekezaji wa aina mbalimbali ukifanyika Zanzibar. Miongoni mwa uwekezaji huo ni ujenzi wa hoteli ya kitalii ya Bawe Island the Cocoon Collection.
Hoteli hiyo ambayo imezinduliwa na Rais Samia wiki hii, imejenhwa kwenye kisiwa kidogo ca Bawe, ambacho ni miongoni mwa visiwa 15 vilivyokodishwa kwa wawekezaji kwa ajili ya miradi ya uwekezaji.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa hoteli hiyo ikiwa ni mwendelezo wa maadhimishi ya miaka 61 ya Uhuru, Rais Samia, alitumia fursa hiyo kuwashukuru wamiliki wa mradi kwa kutimiza ahadi zao kwa mujibu wa makubaliano yao na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Anasema mwaka jana wakati wa maadhimisho ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ndipo liliwekwa jiwe la msingi la mradi huo.
“Binafsi nimefarijika sana kuona uwekezaji kama huo umetekelezwa ndani ya muda na pili kwa kuzingatia miongozo na masharti yanayohitajika ya uwekezaji wa visiwa vidogo vidogo,” anasema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia anasema mradi huo ni mradi wa tatu kuwekezwa na mwekezaji huo, ambapo anamiliki hoteli tatu visiwani Zanzibar.
“Wamewekeza kwenye mradi mitatu na hiyo ni ishara kwamba wawekezaji wetu wanaridhika na mazingira yaliyopo ya kufanya uwekezaji, lakini pia mazingira ya utawala, urasmu umepungua kwa kiasi kikubwa, sheria zimerekebishwa vizuri, hivyo wawekezaji wanavutiwa kuwekeza Zanzibar,” anasema.
Pia anasema mwekezaji huyo amefanya uwekezaji wa dola za kimarekani milioni 42.
” Huo sio uwekezaji mdogo ndugu zangu, nimezunguka nimeona. Kuna uwekezaji wa kutengeneza umeme wa jua, lakini wana mradi wa kuchukua maji ya chumvi, kuyatoa chumvi yote na kufanya maji kwa ajili ya matumizi ya hoteli ndiyo maana gharama imekuwa kubwa mno,” anasema.
Anasema anaamini uamuzi wa wawekezaji hao kufanya uwekezaji huo wa tatu visiwani humo umetokana na uzuri wa visiwa vya Zanzibar pamoja na imani kubwa waliyonayo kwa Serikali na sera zetu nzuri.
Aidha, Rais Samia anasema uongozi ni kuona mbali, hivyo, Rais Mwinyi aliona mbali na kuja na wazo la kukodisha visiwa vidogo vidogo ili viwanufaishe Wazanzibar.
“Tulikuwa na visiwa ambavyo vingeweza kujenga uchumi wa Zanzibar , lakini uchumi tuliukalia, kisiwa hiki kilikuwa kikitumiwa na wavuvi tu.
Walipomaliza kuvua tulichokuwa tunapata kufuata samaki kwenye soko la Malindi, ndiyo faida kuliyokuwa tukipata na kwa vijana kwenda kustarehe.
“Lakini leo hii mradi huu unaleta ajira 400 za watoto wa Kitanzania, umeleta ajira wakati wa ujenzi, umeleta ajira wakati wa uendeshaji, lakini utalipa kodi ndani ya Serikali, utatufanya tukuze mapato, lakini pia utakuza jina la Zanzibar,” anasema na kuongeza;
“Sio muda mrefu Bawe Island itakuwa ikitamba kwenye mitandao na wakieda nje wataimba Bawe Island.”
Anasema ilipotangazwa visiwa hivyo kukodishwa kwa wawekezaji walikuwa wakali kidogo. “Kila kitu kinaonekana hakiwezekani mpaka kifanyike, leo niambieni nani anajuta kuwa na mradi kama huu?” Alihoji Rais Samia na kuongeza;
“Mradi kama huu utaleta ajira, utaleta mapato na utainua jina la nchi yetu Zanzibar,” alisema.
Anasema Maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi Zanzibar, yanawakubusha lengo na dhamira ya Mapinduzi hayo.
Amasema Mpinduzi hayo yalilenga kuondoa ubaguzi na kuwaletea wananchi maendeleo na kustawishi hali zao. “Tupo hapa tumenawili, tunaimba, tumefurahi, tunapendeza, jamani mimi huwa naagalia harusi za Zanzibar.
Jamani ukiangalia harusi za Zanzibar hausemi hiki kisiwa kina maskini. Hakuna na yote ni kazi ya Mapinduzi Matukifu ya Zanzibar. Kwa wale vijana wa zamani ebu chukueni picha za mavazi ya mababu zetu muone leo mambo yalivyo,” anasema Rais Samia kuongeza;
“Ukiangalia harusi ya Zanzibar, hausemi Zanzibar kuna maskini. Yaani ukiangalia watu walivyovaa, zawadi wanazotoka nazo unasema ehee, hii Zanzibar au Ulaya? Mapinduzi yametuletea neema ndugu zangu.”
Aidha, katika mwendelezo huo huo wa maadhimisho ya miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu Zanzibar, Rais Samia alizindua juzi alizindua Shule ya Sekondari Bumbwini Misufini.
Aidha, Rais Samia anapongeza wananchi kwa kuwa tayari kuunga mkono juhudi za Serikali kuwaletea maenedeleo. Pia, Rais Samia alipongeza hatua ambayo wamefikia, akisema hayo ndiyo yalikuwa malengo ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Anasema walikuwa wanaenda hatua baada ya hatua na mwaka jana, wamefika hapo, lakini nako si padogo.
“Wazee wetu waliweka misingi mizuri sana. Waliona jambo la kwanza ni kusoma. Na wazee walivyoleta mapinduzi wakasema ni elimu bure kwa watoto wetu.
Mimi wakati Mapinduzi yanakuja nina miaka minne, bado sijaenda shule,” anasema Rais Samia na kuongeza;
“Mwaka 1965 ndipo nilipoanza kukanyaga banda la Skuli (shule) na nilikuwa sitatimiza umri, Baba yangu alikuwa mwalimu pale Kidoti, akitoka asubuhi natoka naye naingia darasa la kwanza, kwa hiyo mwaka 1965 nilikuwa nasoma darasa la kwanza, lakini mabanda yale ndiyo watoto wetu siku hizi wanaita mabanda ya mbunzi.”
Yalikuwa ya makuti, tulikuwa tunaingia tunasoma, darasa la pili nimesoma Chwaka, angalau yalikuwa na saruji (sakafu) tukaendelea hivyo, lakini baada ya sisi kupewa fursa na wazee tukasoma vizuri, tukajua maana ya elimu, awamu kwa awamu , tumekuwa tukiboresha elimu.”
Anasema waliokuja awamu ya pili wameboresha kwa kiasi chao, awamu ya pili, awamu ya tatu, hivyo hivyo kila awamu inaongeza mpaka wamefikia hatua hiyo.
Anasema ameweza kuingia kwenye madarasa ya shule ya Bumbweni, ndani ameona madarasa ya mtandao.
“Wakati naingia darasani nimekuta watoto wanasoma kwa njia ya mtandao, wameunganishwa na Taasisi ya Elimu Kibaha, darasa linafundishwa kule, wao wanafuatilia huku kila mtu kwa kompyuta yake.
Mapinduzi ni maendeleo hatua baada ya hatua, yale Mapinduzi ya kutafuta Uhuru tulimaliza sasa ni mapinduzi ya kuleta maendeleo na kulinda Uhuru wetu, ndiyo Mapinduzi yetu sasa hivi,” alisema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia anasema ndani ya shule hiyo ameona kuna maabara za kisasa sana. Alisema Fiziki ina maabara yake, Kemia ina maabara yake , vijana wanasoma.
“Huko nyuma tulikuwa tukifanya mitihani form four (kidato cha nne) Zanzibar usiitafute juu, uitafute chini utaiona iko wapi, utakuta ya pili kutoka chini, au imefanya vizuri zaidi ya nne kutoka chini, lakini sababu ilikuwa watoto hawakuwa wakifundishwa sawia, hatukuwa na maabara.
Sasa tumewajengea za kisasa , nilikuwa naongea na walimu mle ndani kwamba hatutaki kusikia ziro wala four (madaraja) .” Anasema
Aidha, anasema wameweka kompyuta darasani sio tu za wanafunzi, bali walimu wazitumie kuboresha ujuzi wao waingie kwenye kompyuta tafute ulimwenguni wanasomeshwaje.
Anasema kwa kufanya hivyo watakuwa walimu bora na maabara hizo zitatumika vizuri.
Rais Samia anasema kabla ya Mapinduzi, Zanzibar na Pemba kulikuwa na shule 62 kati ya hizo za Sekondari zilikuwa tano na shule za awali ilikuwa moja.
“Lakini sasa hivi fikiriani kuna shule za awali ngapi , hiyo ni mwaka 1964. Kipindi hicho wanafunzi waliokuwa shule za awali, shule za msingi na sekondari walikuwa 25, 432, lakini sasa hivi tuna shule 1,308, lakini udahili wetu kwa wanafunzi waliokuwa shuleni mwaka jana (anataja takwimu zaidi 6.5) na kwa mwaka huu idadi utaongezeka,” alisema Rais Samia.
Pia anasema kuna vyuo ambavyo huko nyuma havikuwepo, ambapo anadhani vyuo vikuu Zanzibar wamevipata miaka ya 2000. Alisema sasa hivi wana vyuo vikuu na shule za michepuo na wana mfuko wa kusomesha watoto vyuo vikuu na kumuondea mzazi mzigo wa kusomesha mtoto katika mgazi hiyo.
“Hayo ndiyo matokeo ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, kwani lengo la Mapinduzi ilikuwa ni kustawisha hali za wananchi kielimu, kiafya, wapate maji safi na salama, wapate umeme ili wawe salama waweze kufanya mambo yao kwa salama na kwa amani,” anasema.
Rais Samia anasema hapo walipofikia wana maono ya mbele, ambayo ni kusomesha watoto wawe wataalam na sio tu wasomi. Aliongeza kusema kwamba unaweza ukawa msomi, ulichokisoma hakikusaidii wewe wala Taifa.
Lakini ukiwa mtaalam, huo utaalam utakusaidia wewe na Taifa lako. Alisema kama wasomi watatokea ni vizuri, lakini lengo letu ni kutayarisha wataalam watakaohimiri soko la ajira.
Anasema kwa sasa uwekezaji unaongezeka nchini na jana (juzi) alikuwa Bawe kuna hoteli ya kimataifa imetoa ajira 400, katika ajira zile alikuwa anaangalia watoto wanaofanana na Kipwapwani, kama wapo wachache sana.
“Hiyo inatuambia hatujafanya kazi nzuri sana kuzalisha wataalam katika sekta ya utalii na pengine kulikuwa na changamoto huko nyume, pengine mila zetu,” anasema.
Alisema kuna ajira za kitaalam, ajira za kawaida, lakini badala yake hawakupata wao, wamepata vijana wa Kitanzania.
Anasema kila uwekezaji unaokuja sasa unakuja kwa mitindo ya kutumia mitandao, mawasiliano ni mtandao, oda mtandao, sijui kitanda kimesafishwa ni mtandao, hivyo lengo lao ni kuzalisha vijana watakaoweza kuajirika.
More Stories
Rais Samia anavyotimiza ahadi yake ya kumtua ndoo ya maji mwanamke
Rais Samia anavyozidi kusogeza karibu watoto wa kike na kasi ukuaji teknolojia
Maono ya Rais Samia yanavyozidi kuipaisha Tanzania kupitia utalii