October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Singida Cluster yaondoka na Mbuzi

Na Damiano Mkumbo, Times MajiraOnline, Singida.

TIMU ya Soka ya Singida Cluster imetwaa zawadi ya Mbuzi moja baada ya kuinyuka Singida Youth goli 3-1 katika mchezo wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa Haki ya Mtoto Duniani.

Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Mwenge na kushuhudiwa na watazamaji 2500 wakiwemo watoto kutoka Shirika la Compassion Tanzania, vijana na viongozi mbalimbali, goli la kwanza lilifungwa na Shafii Shabani.

Goli hilo lilidumu dakika zote 45, lakini Singida Youth walikuja juu kipindi cha pili na kufanikiwa kupangua ngome ya washindani wao pale Samwel Jackson aliinua nyoyo zao kwa kufunga goli la kuzawazisha.

Hata hivyo furaha yao haikudumu baada ya Hamisi Salum kuongeza goli la pili kwa Singida Cluster huku Shafii Salum kwa mara nyingine akiwanua mashabiki baada ya kufunga goli la tatu.

Mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi Hamisi Kinga, Nahodha wa Singida Cluster, Hamis Shaban amesema, ushindi huo mnono umetokana na uimara uliotokana na maandalizi ya kutosha waliyoyafanya pamoja na ushirikiano uliwawezesha kutumia nafasi tatu kujipatia magoli.

Akikabidhi zawadi ya ushindi wa mchezo huo ambao ulishuhudiwa pia na wageni kutoka Wizara ya Afya pamoja na viongozi wa Shirika la Compassion International, Mwenyekiti wa Kamati ya Michezo Wilaya ya Singida, Hassan Ngoma aliainisha kuwa michezo ni sehemu ya malezi mema kwa watoto.

Ngoma ambaye pia ni Katibu Tawala wa Wilaya hiyo aliziagiza shule na Taasisi zinazohusika na malezi, kuendelea kuibua na kuimarisha vipaji vya watoto kuanzia umri mdogo ili waweze kuvitumia katika kujenga afya, ushirikiano na kujipatia ajira baada ya kufikisha umri wa ujana.