April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Simbu avunja rekodi ya taifa Boston

-Aibuka wa pili Boston Marathon, avuna zaidi ya shilingi milioni 195.

BOSTON, Marekani.

BINGWA wa dunia wa mbio ndefu, Alphonce Simbu, ameendelea kuipeperusha vema bendera ya Tanzania baada ya kumaliza katika nafasi ya pili kwenye mbio za Boston Marathon 2026 zilizofanyika Aprili 20, 2026 nchini Marekani.

Simbu alionesha kiwango cha juu cha ushindani kwa kutumia muda wa saa 2:02:47 na kufanikiwa kuvunja rekodi ya taifa iliyokuwa ikishikiliwa na Gabriel Geay tangu mwaka 2022, ya muda wa saa 2:03:00.

Rekodi hiyo mpya inamuweka Simbu kwenye orodha ya juu ya wakimbiaji wenye muda bora zaidi duniani kwa sasa.

Mshindi wa mbio hizo alikuwa John Korir kutoka Kenya aliyemaliza kwa muda wa saa 2:01:52, ambapo pia aliweka rekodi mpya ya mashindano katika mbio hizo kongwe na zenye ushindani mkubwa duniani.

Katika ushindani mkali, Simbu alipambana bega kwa bega na mshindani mwingine wa Kenya, Benson Kipruto, ambaye alimaliza katika nafasi ya tatu baada ya mbio zenye kasi kubwa hadi mita za mwisho.

Historia ya mafanikio ya marathoni Tanzania inaendelea kuimarika, ikianzia kwa Juma Ikangaa aliyewahi kuweka rekodi ya saa 2:08:01 mwaka 1989, kabla ya Geay kuivunja mwaka 2022, na sasa Simbu kuipeleka hatua zaidi kwa kiwango kipya.

Kwa matokeo hayo, Simbu amejinyakulia kitita cha dola za Marekani 75,000 (zaidi ya shilingi milioni 195), ikiwa ni mara ya pili mfululizo kupanda jukwaa la ushindi Boston baada ya kushika nafasi ya tatu mwaka 2025.

Kwa ujumla, Simbu ndiye mwanariadha tishio zaidi duniani kwa mbio hizo ndefu, huku akiendelea kuiinua na kuing’arisha zaidi Tanzania katika ramani ya riadha ya kimataifa kwa kasi kubwa.