Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.
WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais,Menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora,George Simbachawene amesema kuwa katika miaka 60 ya Muungano Serikali imeweka utaratibu wa muda wa mgao wa ajira uliokubalika kutumika ambao ni asilimia 79 kwa Tanzania Bara na asilimia 21 kwa Tanzania Zanzibar.
Simbachawene amesema hayo jijini hapa leo,Aprili 15,2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika miaka 60 ya Muungano ambapo amesema, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imekuwa ikifanya kazi na Tume ya Utumishi wa Umma Zanzibar inayoratibu masuala ya ajira kwa watumishi wa umma ili kurahisisha zoezi la kutangaza nafasi za kazi na kuwafikia waombaji walio wengi kwa uharaka zaidi.
“Utaratibu huu unatekelezwa kwa mujibu wa Waraka wa Serikali wa tarehe 10 Mei, 2013,Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imekuwa ikitoa fursa sawa za ajira kwa wananchi wote wa Tanzania ambao wanaomba ajira na kuwa na vigezo stahiki kama elimu, uzoefu na sifa husika,”amesema Simbachawene.
Amesema kuwa katika kuimarisha zaidi muungano,wataalam wa rasilimaliwatu hasa wanaojihusisha na masuala ya ajira kwa nyakati mbalimbali, wamekuwa wakibadilishana uzoefu.
“Ushirikiano huu, umekuwa chachu ya kuendelea kudumisha muungano wetu kwa kupata watumishi wenye sifa na weledi wa kutosha,”amesema.
Aidha amesema kuwa katika kipindi cha miaka 60 ya muungano, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imedhamiria kuondoa changamoto nyingi zinazowakabili waombaji wa fursa za ajira nchini kwa kuendesha usaili wa kuandika/mchujo Kidijitali kwa lengo la kuwafikia waombaji wote mahali popote walipo Tanzania bara na Zanzibar.
Pia amesema ili kukabiliana na changamoto zilizokuwepo, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imesanifu na kujenga mfumo wa kufanya usaili kwa njia ya kielektroniki, mfumo huo umekamilika kwa asilimia 98.
Vilevile amezungumzia Awamu ya Kwanza ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ilianza mwaka 2000-2005 na ilijumuisha maeneo ya utekelezaji 42 ambapo 40 ni ya Tanzania Bara na mawili (2) ya Zanzibar (Unguja na Pemba). Jumla ya miradi 1,704 ya huduma za jamii yenye thamani ya shilingi bilioni 72 ilitekelezwa kupitia mpango huu wa TASAF I.
Ambapo amesema jumla ya miradi 12,347 ya huduma za jamii yenye thamani ya shilingi bilioni 430 ilitekelezwa wakati wa awamu hii ya Pili ya TASAF (TASAF II).
“Moja kati ya shughuli kuu za Mpango wa TASAF III kipindi cha kwanza ilikuwa ni utoaji wa ruzuku kwa kaya za walengwa. Katika kipindi cha kwanza, kiasi cha shilingi billioni 968.7 zilikuwa zimehawilishwa kwa kaya za walengwa zipatazo 1,118,752 katika vijiji, mitaa na shehia 9,831,”amesema.
Ameeleza kuwa Katika kipindi cha pili hadi kufikia Juni 2023, kiasi cha shilingi bilioni 696.7 zimehawilishwa kwa kaya za walengwa zipatazo 1,371,916 katika vijiji, mitaa na shehia 17,260.
“Vile vile mpango katika kipindi cha pili cha awamu ya tatu ilitekeleza afua ya kukuza uchumi wa Kaya ambayo inahusiana na uhamasishaji wa uundaji wa vikundi vya kuweka akiba na kuwekeza kwenye miradi ya uzalishaji mali. Vikundi 46,569 vyenye wanachama 627,508 vilianzishwa,”amesema.
Ameeleza kuwa Katika kipindi cha miaka 60 ya muungano, mpango wa TASAF umekuwa na manufaa makubwa mathalani katika eneo la uhawilishaji wa ruzuku kwa walengwa ambapo kiasi cha shilingi bilioni 824.4 kililipwa kwa Kaya Maskini 1,321,098 Tanzania Bara na shilingi bilioni 41.2 ililipwa kwa kaya maskini 50,818 Zanzibar.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa