Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Gulwe
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi George Simbachawene ameshauri kujengwa kwa mabwawa ya kisasa maeneo ya milimani katika vijiji vya Iyenge,Ludi,Vibewele na Mzogole wilayai Mpwapwa,ili kuzuia athari ya mafuriko ambayo yamekuwa yakisababisha kusombwa kwa reli ya kati na uharibifu wa makazi ya watu.
Simbachawene ambaye pia ni Mbunge wa Kibakwe wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma ametoa ushauri huo wakati wa ziara ya Waziri Mkuu Dkt.Mwigulu Nchemba, aliyefika kijijini Gulwe Jimbo la Kibakwe kukagua uharibifu wa miundombinu ya reli na makazi ya watu uliosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha.

Amesema yapo mabwawa yaliyojengwa zamani wakati wa teknolojia finyu na kwamba sasa yanahitajika mabwawa yatakayojengwa kwa teknolojia za kisasa maeneo ya milimani tofauti na yaliyopo.
Simbachawene amesema tatizo lipo milimani maji yanakotoka hivyo ni vyema mabwawa yakajengwe huko ili maji mengi yaishie hukohuko.
”Ni vyema wataalamu wakaangalia namna maji yanavyoweza kupunguzwa kule milimani kwa kuingia kwenye mabwawa ili huku chini yaje kidogo,”amesema Simbachawene.
Vile vile ameshauri kujengwa kwa kituo cha afya ili kusaidia matibabu kwa wananchi wa eneo hilo pamoja na abiria wanaokwama kusafiri pindi reli ya kati inapokuwa imeathiriwa na mvua .
Awali Waziri Mkuu Dkt.Nchemba ametoa maelekezo kwa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS),kufanya makadirio ya hali ya dharura ili kujua kiasi kinachohitajika katika daraja la Godegode na korongo la Gulwe yalioathiriwa na mvua kwa ajili ya kuanza ujenzi wa miundombinu hiyo iweze kupitika.
sanjari na hayo Dkt.Nchemba amewataka wananchi kutunza mazingira ili kupunguza ama kumaliza kabisa athari zinazosababisha mafuriko.
”Ni lazima tuambiane ukweli katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,tunapaswa kubadilika ili tupunguze madhara,watu wasijenge kwenye mkondo wa maji,tusiharibu mazingira kwa kukata miti,tusilime kilimo kisichozuia mtiririko wa mchanga,”amesema Dkt.Nchemba.

Pia amesema,anatambua changamoto ya barabara ya Mpwapwa -Gulwe ambapo amedai kuwa mkandarasi ameishapatikana kinachosubiriwa ni kupata fedha tu.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule,amesema huo ni moja ya mikoa yenye maeneo yanayoathiriwa na mvua ikiwa ni pamoja na vijiji vya Mtanana na Fufu huku akisema shilingi bilioni 64 zilitolewa na Serikali na kutumikia kurekebisha maeneo yaliyoathirika.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi