Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online, Dodoma
Serikali imesema itaendelea kudumisha amani, mshikamano na utulivu kama siri ya mafanikio ya maendeleo na ustawi wa watanzania wote pamoja na kuhakikisha shughuli za uzalishaji zinafanyika katika mazingira salama.
Kauli hiyo ilitolewa Aprili 13, 2022 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu George Simbachawene Bungeni, Jijini Dodoma wakati wa kuhitimisha hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Waziri Simbachawene alihimiza kudumisha upendo licha ya uwepo wa changamoto mbalimbali za majanga ya Dunia wananchi hawana budi kuendeleza umoja wakati serikali inaendelea kufanya jitihada za kukabiliana na changamoto hizo.
“Nitoe rai pamoja na changamoto tunazozipata katika kipindi hiki cha majanga ya Dunia ambapo Tanzania hatuko peke yetu tusivunje umoja wetu, tusivunje mshikamano wetu tuendelee kushirikiana, kupendana na kuhakikisha zile changamoto tunajadiliana na kukubaliana kwa pamoja ili tuweze kusonga mbele kwa mafanikio makubwa,”Alisema Waziri Simbachawene.
Aidha alipongeza hatua ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kujenga uhusiano na ushirikiano na mataifa mengine Duniani na namna anavyosaidia kuitangaza Nchi kimataifa.
“Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ametupa unafuu na wepesi katika kuielezea Tanzania lakini amekuwa na bahati katika kuifanya Tanzania kujulikana kimataifa kama taifa la watu wastaarabu na Taifa linaloendelea,”Alipongeza.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi