Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Mpwapwa
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Jimbo la Kibakwe,George Simbachawene ametoa wito kwa Watanzania wenye sifa za kujiandikisha katika Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kujitokeza kwa wingi katika vituo ili kupata Kitambulisho cha Mpiga Kura kitakachowawezesha kupata haki ya kuchagua Viongozi katika Uchaguzi Mkuu ujao .
Simbachawene amewataka Watumishi wa Umma nchini kuhakikisha wanatumia haki yao kujiandikisha kwenye daftari hilo ili kuwawezesha kuchagua viongozi akiwemo Rais, Wabunge pamoja na Madiwani kwenye uchaguzi huo .
Waziri Simbachawene ametoa wito huo leo Jumatatu,Disemba 30,2024 mara baada ya kuboresha taarifa zake kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Kituo cha Wapiga Kura kilichopo Kata ya Pwaga Wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma.
Amesema kitendo cha kwenda kuboresha taarifa katika kituo husika kwa Mtumishi wa Umma ni kujihakikishia usahihi wa taarifa zake pamoja na uhakika wa mahali atakapopigia kura.
“Nimefika hapa ndani ya muda mfupi nimeboresha taarifa zangu ambapo nimepata kitambulisho kipya kitakachoniwezesha kutumia haki yangu ya kidemokrasia muda utakapowadia wa kuchagua na kuchaguliwa”amesema Waziri Simbachawene.
Katika hatua nyingine Simbachawene ameipongeza Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuboresha zoezi hilo na kufanya kazi kwa weledi inayoimarisha Demokrasia nchini huku akisifu jinsi zoezi hilo linavyoendesha kwa umakini na uharaka ili kuwawezesha wananchi to go kuendelea na shughuli zingine za kujiingizia kipato
Simbachawene amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa kuendelea kuimarisha Demokrasia nchini na kuendelea kuiwezesha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Awali, Mwandikishaji wa Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Kituo hicho Christina Chigohe ameeleza kuwa zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linafanyika kwa siku saba ambapo lilianza Disemba 27 na litafikia tamati Januari 2, 2025.
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unaoendelea unaongozwa na kaulimbiu “Kujiandikisha kuwa Mpiga Kura ni Msingi wa Uchaguzi Bora”.
More Stories
Wananchi wa Ikuvilo watakiwa kujitokeza kuhakiki taarifa zao
Watanzania wahimizwa kutenda mema
Nani kuwa mrithi wa Kinana CCM?