*Wizara yatanabaisha miradi yake
*Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia waendelea kusambazwa
Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene ametembelea mabanda ya Wizara ya Nishati na Taasisi zake katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Ufunguzi wa maadhimisho hayo ulifanyika leo Juni 19,2024, ambapo Waziri Simbachawene ndio aliyekuwa mgeni rasmi katika ufunguzi huo.
Akiwa katika Banda la Wizara ya Nishati, Simbachawene alipokelewa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Neema Mbuja ambaye alimweleza kuhusu miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa na Wizara.
Pia alimuelezea miradi inayotarajiwa kutekelezwa, lengo kuu likiwa ni kuhakikisha nchi inakuwa na nishati ya kutosha kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo majumbani, viwandani, magari na taasisi.
Aidha, akiwa katika Banda la Wizara hiyo Simbachawene ameelezwa kuhusu utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia ikiwa ni jitihada za Serikali kuhakikisha kuwa wananchi wanaachana na matumizi ya nishati isiyo safi na kutumia nishati iliyo safi na salama.
Hata hivyo Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Nishati, amemkabidhi Simbachawene nakala za Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha kuwa Mkakati huo unafika kwa makundi mbalimbali ya wananchi.
Viongozi wengine walioambatana na Simbachawene ni Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwan Kikwete na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua