January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Simbachawene aipongeza e-GA usimamizi wa Tehama Serikalini

Na Mwandishi wetu,Timemsjira online,Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, ameipongeza Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa jitihada kubwa inazozifanya katika kukuza na kuimarisha Serikali Mtandao nchini.

Simbachawene alitoa pongezi hizo jana, alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Mamlaka  ya Serikali Mtandao zilizopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, kwa lengo la kukagua utekelezaji wa majukumu ya e-GA katika usimamizi wa matumizi ya TEHAMA kwenye taasisi za umma.

Alisema kuwa, kuimarika kwa matumizi ya TEHAMA katika taasisi za umma, kunatokana na usimamizi mzuri wa e-GA katika kuimarisha jitihada za serikali mtandao, hali ambayo imesaidia kuongezeka kwa ufanisi wa utendaji kazi wa shughuli za serikali pamoja na utoaji huduma kwa wananchi.

“Bila Serikali Mtandao mambo mengi yangekuwa hayaendi sawa, e-GA mmetumia teknolojia kurahisisha na kufanikisha shughuli nyingi za Serikali kufanyika kwa wakati pamoja na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, nawapongeza sana”, alisema.

Pamoja na pongezi hizo, pia Waziri aliitaka e-GA kuimarisha Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (eGovRIDC) ili kutengeneza vijana wengi zaidi ambao watabuni mifumo inayotatua changamoto zilizopo. 

“Ni muhimu kuimarisha kituo cha utafiti na ubunifu ili kuandaa na kutengeza vijana mahiri katika masuala ya teknolojia kwa maslahi mapana ya taifa, na sisi upande wa Wizara tutahakikisha tunatoa msaada wa kutosha pale mtakapohitaji”, alisema.

Aidha, aliitaka e-GA kuendelea kuwajengea uwezo watumishi wake kwa kuhakikisha wanapata mafunzo ya muda mfupi na mrefu kutoka ndani na nje ya nchi, ili kuwaongeza ujuzi wa kukabiliana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia katika usanifu wa mifumo, miundombinu pamoja na miradi ya TEHAMA yenye tija kwa taifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu e-GA Eng. Benedict Ndomba, alimshukuru Waziri kwa kufanya ziara hiyo pamoja na ushirikiano mkubwa anaoupata kutoka Wizarani katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi.

Aidha alisema kuwa, e-GA itaendelea kuimarisha kituo cha utafiti na ubunifu pamoja na kutoa elimu kwa Taasisi za Umma katika usimamizi na uzingatiaji wa Sheria, kanuni, viwango na miongozo ya Serikali Mtandao ili kuhakikisha mifumo na miradi yote ya TEHAMA katika taasisi za umma inakuwa na tija kwa taifa.