Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Sumbawanga
KIKOSI cha klabu ya Simba kimefanikiwa kutwaa ubingwa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (Azam Sports Federation Cup) baada ya kuwafunga Namungo FC goli 2-1 katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Nelson Mandela uliopo Sumbawanga Mkoani Rukwa.
Ushindi huo unaifanya Simba kuweka historia mpya kwenye mashindano hayo kwa kuwa timu ya kwanza kubeba taji hili mara mbili toka mashindano hayo yaliporejeshwa tena msimu wa 2015/16 na kuzipiku timu za Yaynga, Azam na Mtibwa ambazo tote zimechukua mara moja.
Lakini pia wakati Simba imetwaa ubingwa huo kwa mara ya kwanza katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Jamhuri Dodoma iliwafunga Mbao FC goli 2-1 .
Mbali na rekodi hiyo lakini pia klabu hiyo iliyofanikiwa kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) inavijua kutwaa ubingwa huo wa tatu baada ya kuanza msimu huu kwa kutwaa Ngao ya Hisani baada ya kuwafunga Azam FC goli 4-2.
Katika mchezo huo ambao ulitabiriwa kuwa na ufundi mwingi ambao pia ulianza kwa kasi huku timu hizo zikishambuliana kwa zamu, Simba ilipata pigo dakika ya 25 baada ya kiungo wake Francis Kahata kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo na nafasi yake ikachukuliwa na Hassan Dilunga.
Dakika mbili baadaye Simba ilipata goli lililofungwa na Luis Miquissone akimalizia mpira uliookolewa na beki Carlos Protas baada ya krosi iliyopigwa na Shomari Kapombe.
Goli hilo la kuongoza liliwafanya Simba wazidi kujiamini na kuongeza kasi ya mashambulizi kwenye lango la wapinzani wao lakini hawakuweza kuzitumia vema nafasi walizotengeneza.
Dakika ya 39 Nahodha John Bocco alifanikiwa kuipatia timu yake goli la pili kwa kichwa akimalizia pasi ya kichwa ya Miquissone aliyepokea krosi kutoka kwa Clatous Chama na kwenda mapumziko wakiongoza.
Kipindi cha pili Namungo waliingia wakionekana wanataka kupata magoli huku Simba wakitaka kuongeza, dakika ya 56 beki Edward Manyama akaifungia Namungo FC bao la kufutia machozi akimalizia mpira wa kona uliopigwa Abeid Athumani.
Kama ilivyokuwa kwa Simba, goli hilo liliamsha morali ya wachezaji wa Namungo ambao walianza kulishambulia kwa kasi lango la Simba ambao nao walifanya majaribio kadhaa kwa wapinzani wao bila mafanikio na dakika 90 kumalizika Simba wakishinda goli 2-1.
Katika mchezo huo wa fainali, Miquissone alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mechi, Chama akitwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mashindano wakati zawadi ya Mfungaji Bora ikichukuliwa na Omary Yassin wa Panama aliyefunga goli tisa.
Baada ya mashindano hayo, timu hizo zinasubiriana tena kwenye mchezo wa Ngao ya Hisani utakaochezwa Agosti 29 kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid uliopo Arusha.
Akizungumza mara mchezo huo wa fainali, rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) Wallece Karia amesema, mapendelezo mchezo huo kuchezwa Arusha yalitolewa kwenye kikao Kamati ya Utendaji kilichotumika kupitisha mambo mbalimbali ikiwemo kumuongea mkataba Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao, Mkurugenzi wa Ufundi na Mkurugenzi wa mashindano baada ya kuridhishwa na utendaji wao.
“Tulipokea mapendekezo ya Kamati ya Mashindano kuhufu tuzo za VPL lakini mchezo wa Ngao ya Hisani wa Agosti 29 kuchezwa Arusha na sisi tumekubaliana nao ambao utawakutanisha tena Simba na Namungo kwa mujibu wa kanuni, ” amesema Karia.
Kikosi cha Simba: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Kennedy Juma, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Luis Miquissone, Gerson Fraga ‘Viera’, John Bocco, Clatous Chama na Francis Kahata/Hassan Dilunga dk27.
Namungo FC: Nourdine Balora, Rodgers Gabriel, Edward Manyama, Steven Duah, Carlos Protas, Hamisi Khalfan, Hashim Manyanya/Frank Mkumbo dk60, Daniel Joram/Steven Nzigamansabo dk46, Bigirimana Blaise, Lucas Kikoti na Abeid Athumani.
More Stories
15 wajinoa Juventus,akiwemo mtoto wa Mwenyekiti wa CCM Mbeya
Za Kwetu Fashion Show, yawapaisha wanamitindo nchini
TCAA yaadhimisha siku ya usafiri wa anga Duniani kwa kushiriki mbio za Marathon UDSM