December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Simba yawapa tahadhari JKT Tanzania

Na Yusuph Digossi, TimesMajira Online

KOCHA mkuu wa Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) Simba, Sven Vandenbroeck ni kama amewatangazia hali ya hatari Maafande wa JKT Tanzania ambao watakutana nao Oktoba 4 katika uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Simba ambayo inashika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu wakiwa na alama 10, watakutana na Maafande hao ambao leo watakuwa ugenini kuvaana na wenyeji Coastal Union.

Tahadhari hiyo imetolewa mara baada ya mchezo wao wa juzi waliopata ushindi wa goli 3-0 dhidi ya Gwambina FC, ambapo Sven amehitaji mambo mawili kutoka kwa wachezaji wake.

Jambo la kwanza analohitaji ni kuona wachezaji wake wanaonesha kiwango kizuri kama kilichooneshwa katika mechi zao za mbili za nyumbani lakini pia kucheza zaidi kitimu hadi mwisho wa msimu ili kuwapa manufaa katika mashindano ya Klabu bingwa.

Ingawa kiufundi kutakuwa na mabadiliko ya kiuchezaji kutokana na aina ya uwanja watakaoutumia lakini kocha huyo amesema anatarajia kuona morali ya kupambana ya hali ya juu kwa wachezaji wake ambayo itawapa pointi tatu.

Amesema, kama wameweza kutengeneza nafasi nyingi za magoli na kupata ushindi dhidi ya timu iliyokuwa vizuri kiufundi, basi anaamini mchezo ujao pia wataweza kupata alama tatu muhimu.

Mbali na kutoa maagizo hayo kwa wachezaji wake, lakini kocha huyo amefurahishwa na viwango vinavyoonyeshwa na wachezaji wake jambo ambalo litamrahisishia kazi katika michuano ya kimataifa.

Kinachomfurahisha na kumpa matumaini ya kufanya vizuri katika mechi zao za mbeleni ni kuona kila mchezaji anayepata nafasi ndani ya kikosi chake anauwezo wa kufunga.

“Inafurahisha kuona washambuliaji wote wana uwezo mkubwa wa kufunga lakini si washambuliaji pekee bali kila mchezaji ndani ya kikosi changu anauwezo wa kufunga pale anapopata nafasi. Naamini hili ni jambo zuri kuelekea kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika,” amesema Sven.

Hata hivyo kocha huyo ameendelea kuwasisitiwa wachezaji wake kupambana kuonesha uwezo ili kupata nafasi kwani msimu huu kila mchezajin aliyenaye ni mzuri na wanaohitajika ni 11 hivyo ni lazima kupambania namba katika kikosi.