December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Simba yataka rekodi ya kibabe kwa Ihefu

Na Ester Macha, TimesMajira Online Mbeya

UONGOZI wa klabu ya Simba umeapa kuweka rekodi ya aina yake jijini Mbeya katika mchezo wao wa kwanza wa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) dhidi ya wenyeji wao Ihefu utakaochezwa Septemba 6 katika uwanja wa Sokoine.

Kwa misimu kadhaa timu hiyo imekuwa ikipata ushindi mnono katika mechi zao za kwanza za msimu na safari hii wanachokitaka ni kuvunja rekodi zao zote walizoziweka miaka ya nyuma.

Tayari kikosi cha timu hiyo chini ya benchi la ufundi linaloongozwa na Sven jana kimeanza maandalizi kuelekea kwenye mchezo huo muhimu kwao.

Simba watakwenda kukutana na Ihefu huku wakiwa na morali ya hali ya juu baada ya kushinda mechi zao zote walizocheza kama sehemu ya maandalizi ya msimu mpya ikiwemo ule wa maadhimisho ya ‘Simba Day’ dhidi ya Vital’O ya Burundi waliopata ushindi wa goli 6-0.

Pia timu hiyo ilipata ilifanikiwa kutwaa taji la Ngao ya Jamii kwa msimu wa nne mfululizo baada ya kuwafunga Namungo FC goli 2-0 katika uwnaja wa Sheikh Amri Abeid ya kuweka historia kwa kuwa timu iliyotwaa taji hilo mara sita.

Akizungumzia maandalizi ya kikosi chao, Meneja wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu amesema kuwa, kikosi chao kimeenza maandalizi kikiwa kamili na watahakikisha wanaanza na ushindi mnono mbele ya wenyeji wao.

Amesema, safari hii wanataka mambo kuwa tofauti na kuanzika rekodi mpya kwa kuanza na ushindi wa kishindo ambao utawawezesha kuanza msimu huku wakiwa kileleni mwa msimamo wa Ligi.

“Kwa zaidi ya miaka minne tumekuwa tukianza na ushindi wa kishindo katika mechi zetu za kwanza lakini safari hii tunahitaji rekodi mpya na tunajipanga kuhakikisha mkakati wetu unafanikiwa,” amesema Rweyemamu.

Mbali na kutaka rekodi hiyo, msimu huu huenda ukawa wa tofauti kwa timu hiyo baada ya Sven kuweka wazi ni lazima wafanye kazi ya ziada kwani ni wazi msimu utakuwa mgumu ukilinganisha na msimu uliopita.

Jambo hilo limewafanya viongozi wa benchi la ufundi la klabu hiyo kutumia mbinu mbalimbali za kiufundi ambazo zitawafanya kupata muunganiko mzuri zaidi ambao pia utawanufaisha katika mashindano ya Ligi Mabingwa Afrika.

“Ligi itakuwa ngumu kwani timu zimesajili wachezaji wazuri hivyo tumejipanga kuonesha ushindani mkubwa zaidi hata ya msimu uliopita ili kutwaa tena taji la Ligi,”.

Katika hatua nyingine, Vandenbroeck ameweka wazi kuwa hana tatizo lolote na mshambuliaji Meddie Kagere kama taarifa mbalimbali katika mitandao ya kijamii zinavyoeleza.

Siku mbili zilizopita katika mitandao mbalimbali ya kijamii watu wamekuwa wakidai kuwa Mfungaji Bora kwa misimu miwili mfululizo aliyefanikiwa kufunga goli 45 alitofautiana na kocha wake hali iliyopelekea kukunjana.

Lakini jana katika mtandao rasmi wa klabu hiyo, Sven amesema kuwa
“Siwezi kutumia nguvu kwenye mambo yasiyo ya maana ambayo sijui yanatoka wapi. Mimi sina tatizo, Meddie hana tatizo hilo ndilo ninaweza kusema,”.