November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Simba, Yanga ni ubabe wa pesa usajili wa dirisha dogo

Na Iddy Lugendo, TimesMajira Online

WATANI wa jadi Simba SC na Yanga SC wameendelea kutunishiana misuli kwenye usajili wa dirisha dogo kila mmoja akiendelea kuimarisha kikosi chake ili kuhakikisha wanafanya vyema katika michuano ya Ligi ya mabingwa na kombe la shirikisho barani Afrika na ligi za ndani (ligu ya Tanzania bara NBC na kombe la shirikisho la Azam).

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania, Yanga SC wamemtambulisha mshambuliaji Mzambia, Kennedy Musonda kutoka Power Dynamos ya kwao kuwa mchezaji wao mpya.

Huo unakuwa usajili wa pili tu katika dirisha hili dogo kwa Yanga, washindi wa mataji yote msimu uliopita pamoja na Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) na Ngao ya Jamii ambayo pia wametwaa na msimu huu- baada ya kiungo Mzanzibari, Mudathir Yahya Abbas.

Musonda mwenye umri wa miaka 28 pia amechezea timu za Green Eagles, Nakambala Leopards na Lusaka Dynamos zote za kwao na kwa sasa ni mchezaji wa timu ya taifa ya Zambia.

Hatua hiyo inazidi kuwa matumaini mashabiki na wanachama wa klabu ya Yanga wakiamini kuwa viongozi wa timu hiyo wamedhamiria kuhakikisha wanatetea ubingwa wao na kufanya vyema kwenye michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika baada ya kufuzu hatua ya makundi huku watani wao nao wakiwa makundi ya klabu bingwa barani Afrika (CAF)Hivyo, Simba SC imeshusha mkata umeme kiungo wa ulinzi wa Kimataifa wa Burkina Faso, Hamed Ismael Sawadogo kuwa mchezaji wake mpya katika dirisha hili dogo.

Sawadogo anakuwa mchezaji mpya wa pili katika dirisha hili dogo baada ya kiungo mshambuliaji wa Kimataifa wa Burundi, Saido Ntibanzokiza aliyekuwa anacheza Geita Gold baada ya hapo alikuwa anawatumikia Yanga.

Sawadogoni (26) anajiunga na Simba SC kutoka Difaâ El Jadida ya Morocco baada ya awali kuzitumikia Enppi SC ya Misting, Al-Arabi SC ya Kuwait, Al Mabarra ya Lebanon, AS Douanes, US Ouagadougou, Salitas na RC Kadiogo za kwao.

Kwa sajili hizi kutoka kwa miamba hiyo ya soka la Tanzania Simba na Yanga wamedhamiria kuhakikisha wanafanya vyema katika michuano yote iliyopo mbele yao hii ikidhihirisha kabisa mabosi hao wameamua kuvunja benki na kushusha vifaa vya maana ili kuja kuzipa mafanikio miamba hiyo.