January 26, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Simba yamvulia kofia Rais Samia, yamuahidi makubwa dhidi ya Horoya.

Na mwandishi wetu, TimesMajira Online

Wakati timu ya Simba ikiibuka na ushindi wa bao 3-0 dhidi ya Mtibwa Sugar ya Turiani mkoani Morogoro, uongozi wa klabu hiyo umesema ni jambo zuri kuwa na Rais wa nchi anayependa michezo kiasi cha kuongeza motisha katika utafutaji magoli muhimu ya kuzivusha timu za nchi yake kwenye michuano ya Kimataifa.

Hayo yamekuja kutokana na ofa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoa Sh Milioni 5 kila goli litakalopatikana kwa timu za Simba na Yanga, Simba ikishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati mtani wao wa jadi Yanga, akicheza Kombe la Shirikisho.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Msemaji wa Simba, Ahmed Ally, amesema si tu Rais Samia anatamani timu za Tanzania zifanye vizuri Kimataifa, bali pia anashiriki kikamilifu katika mbinu ya utafutaji wa magoli muhimu ya kuzisaidia timu za nchi yake.

Amesema hali hii inaongeza chachu ya wachezaji, mashabiki, wanachama na viongozi wote kuona wana deni kubwa kwa rais wao, hivyo kuongeza bidi kubwa kushinda kwenye mechi zao.

“Si tu Rais Samia anataka twende mbele, bali pia anaingia kwenye watafutaji wa magoli, kwa maana kununua goli katika mechi ngumu kama hizi, anamaanisha anataka wachezaji wacheze jihadi ili kuyapata kwa lengo moja tu timu ishinde na kupata pointi muhimu.

“Mambo kama haya kufanywa na mtu mkubwa kama Rais wa nchi yanatia moyo, ukizingatia anayefanya haya si mtu wa kawaida isipokuwa raia namba moja kwenye Taifa letu, hivyo sisi Simba tunamuahidi makubwa mama yetu kwenye mechi yetu dhidi ya Horoya Jumamosi ijayo kwa lengo moja la kufuzu robo fainali,” Alisema Ally.

Katika michuano ya Kimataifa inayoshirikisha timu za Simba na Yanga, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amejitokeza kununua kila goli litakalopatikana kwa Sh Milioni 5, ambapo mpaka sasa Yanga wamevuna milioni Milioni 30 kwa kufunga bao 6, huku Simba wao wakipata Sh Milioni 10 kwa kufunga mabao 2.