Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online DSM
MABINGWA watetezi wa ngao ya jamii Tanzania bara timu ya Simba imeendelea kujiimarisha katika kuhakikisha wanakuwa mabingwa wa ndani na nje ya uwanja kwa msimu huu wa 2023/2024 klabu hiyo inategemea kuvuna jumla ya shilingi milioni mia tano ikiwa ni sehemu ya faida kutoka katika makusanyo ya shilingi bilioni 25,930,722,300 ambapo matumizi yanategemewa kuwa kiasi cha shilingi bilioni 25,423,997,354.
Aidha, Malengo ya klabu ya Simba ni kujenga timu imara yenye uwezo wa kushinda makombe, kujenga taasisi imara na endelevu, kujenga chapa imara ndani na nje, ya Tanzania, kujenga misingi imara na yenye tija kwa wanachama na wapenzi, kujenga uwezo wa kifedha ili kufikia malengo, kuvutia wafanyakazi wenye weredi, kujenga misingi imara ya mawasiliano na matawi/wanachama.
“Tumefanya maboresho makubwa kwenye benchi la ufundi tukianzia na kocha nadhani wote mnaona. Tumeboresha idara ya afya ya timu yetu, tuna madaktari bora sana. Lakini pia tumeimarisha timu ya vijana kwa kutafuta vijana kutoka maeneo mbalimbali nchini. Timu yetu ya wanawake imekuwa bora sana. Eneo lingine ni tumeimarisha uhusiano kwa kiasi kikubwa na wadhamini wetu. Sehemu nyingine kubwa ni kushinda Ngao ya Jamii mbili na kuwa mashabiki bora wa AFL. Simba ilileta Rais wa FIFA na kubwa zaidi kuitangaza Tanzania.” CEO Imani Kajula
“Tunataka kuwa mabingwa wa ndani na nje ya uwanja. Tulianzisha WhatsApp channel wakawa wanatusema lakini leo hii tunaongoza kwa kuwa namba moja Afrika Mashariki na Kati na walikuwa wametuzidi YouTube lakini hivi ninapoongea sasa tumewapita na tunaongoza kwenye mitandao yote.”
“Tutaendelea kujenga rasilimali za Simba na eneo lingine ni kuwa na wafanyakazi wenye weledi na uwezo mkubwa sana. Mbele tunaangalia kuboresha mapato, kuimarisha biashara ya jezi, Sandaland amefanya yale mliyokuwa mnayataka kama jezi kutoka mapema na jezi yenye ubora. Ni mzabuni aliyetimiza malengo yenu wanachama. Mwaka huu tunaangalia namna ya kushirikisha matawi katika uuzaji wa jezi ili kuwaongezea mapato.”
“Changamoto zilizopo ni rasilimali fedha, kuongezeka kwa gharama za uendeshaji, kutanuka kwa mahitaji, kuumia kwa wachezaji, mabadiliko na ushindani kuongezeka na kuendelea kuwa timu namba moja.”- CEO Imani Kajula.
Naye Mwenyekiti wa Simba Murtaza Mangungu amesema Simba imeshafanya mambo mengi makubwa, yaliyopita, yanayofanyika sasa na mengine yanakuja,sisi mliotupa dhamana tupo tayari kupokea maoni ambayo yataipeleka Simba mbele na Lengo letu ni kujenga umoja. Mfano mtu anasema uwekezaji hauna faida wakati kabla ya uwekezaji mapato yalikuwa Tsh. 1.6 bilioni, mara baada ya uwekezaji yamepanda hadi Tsh. 6.9 bilioni. Afrika tulikuwa nafasi zaidi ya 80 kwenye ubora na sasa tupo nafasi ya saba. Tunataka ukosoaji wenye tija.
“Kama mnakumbuka mlichanga pesa kwa ajili ya ujenzi wa uwanja na pesa ile ilitumika kujenga ukuta wa uwanja wa Bunju na pesa zingine zilitumika kuimarisha kambi ya timu, Tujenge Simba imara kwa kizazi cha sasa na baadae. Tuendelee kushirikiana na naamini Mwenyezi Mungu atatutangulia. Mkutano umefunguliwa.”- Mwenyekiti wa Klabu, Murtaza Mangungu
Nicolas Mihayo akimwakilisha Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo nchini (BMT) amesema tunawapongeza Simba kwa kufuata malekezo ambayo ilipewa kufanyia kazi katika mapendekezo ya marekenisho ya katiba. Hili ni jambo la mfano kwa timu zingine. Serikali inawapongeza na inawatakia kila la kheri.
Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Simba, Jaji mstaafu Thomas Mihayo amesema Kutofautiana ni jambo la kawaida, jambo la msingi ni namna gani ya kutatua changamoto maana kuna mengine yanaweza kuwa kweli na mengine sio kweli na zikitokea tofauti zisiingie kwenye timu. Mtu yoyote asiyeitakia mema Simba huyo ni msaliti.
More Stories
Watakaokwamisha mapato Kaliua kukiona cha moto
Dkt.Gwajima aagiza kuundwa kamati za ulinzi wa watoto
Kilo 673.2,dawa za kulevya zakamatwa Bahari ya Hindi