Na Yusuph Digossi, TimesMajira Online
VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL), Simba leo watakuwa katika uwanja wao wa nyumbani kusaka alama tatu muhimu katika mchezo wao namba 245 utakaochezwa kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa dhidi ya wapinzani wao Dodoma Jiji FC.
Simba itaingia katika mchezo ikiwa na lengo la kutaka kuendeleza ubabe kwa Dodoma ambao walikubali kichapo cha goli 2-1 katika mchezo wa Februari 4 huku Jiji nao wakitaka kulipa kisasi kwa kuondoka ana alama zote tatu.
Mbali na kutaka kuendeleza ubabe Simba inahitaji zaidi alama hizo ili kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa Ligi ambapo wanaongoza wakiwa na alama 58 wakiwazidi alama moja Yanga ambao wapo nafasi ya pili huku Azam ikiwa nafasi ya tatu na alama zao 54.
Kocha msaidizi wa Simba, Seleman Matola amesema kuwa, baada ya kuchukua alama zote tisa katika mechi zao za Kanda ya Ziwa sasa wanahamishia nguvu katika mchezo huo ambao wanahitaji alama zote tatu ili kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa Ligi.
Kama timu wapo vizuri na hesabu zao ni kutetea tena ubingwa wao kwa msimu wa nne mfululizo hivyo hauwezi kuchukua ubingwa kama unashindwa kuchukua alama tatu katika kila mchezo ulio mbele yako.
Matola amesema kuwa, wanatambua kuwa mchezo huo hautakuwa rahisi kwani wapinzani wao wataingia uwanjani na dhamira ya kutaka kulipa kisasi baada ya kikosi chao kuondoka na alama zote tatu katika mchezo wao wa kwanza.
“Ukiangalia jinsi walivyocheza na Azam katika mchezo wao wa mwisho ni wazi kuwa Dodoma wana timu nzuri tena yenye ushindani na ndio maana tumejiandaa vilivyo kuhakikisha tunaendelea kuwa bora katika uwanja wetu wa nyumbani na kuchukua alama zote tatu,” amesema Matola.
Nahodha msaidizi wa Simba, Mohammed Hussein Tshabalala amesema kuwa, tayari benchi la ufundi limeshamaliza kazi yao na sasa kilichobaki ni wachezaji kuamua matokeo ndani ya dakika 90.
Watahakikisha wanafuata maelekezo yote waliyopewa na viongozi wao na kinachowapa matumaini ya kupata matokeo mazuri ni morali waliyonayo baada ya kubeba alama zote tisa katika mechi zao tatu za ugenini na kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi.
“Benchi letu la ufundi, viongozi na mashabiki walitutuma kazi Kanda ya Ziwa ambayo tuliifanya vizuri na sasa tunarudi katika dimba letu la nyumbani hivyo tunawaomba wapenzi wa Simba wajitokeze kwa wingi kutupa sapoti ili kufanikiwa kuondoka na alama zote tatu,” amesema Tshabalala.
Kwa upande wake kocha msaidizi wa Dodoma Jiji FC, Renatus Shija amesema kuwa, mkakati watakaoingia nao katika mchezo huo wa leo utawaacha midomo wazi wenyeji wao kwani hawataaamini kwa kile watakachokutana nacho.
Amesema, kwa sasa mkakati wao mkuu ni kukusanya alama sita ambazo zitawawezesha kufikisha alama 44 ambazo zitawahakikishia kusalia ndani ya Ligi Kuu msimu ujao.
“Ushindi wa leo ni muhimu sana kwetu kwani tutakuwa tumebakiza alama tatu pekee ili kuwa huru. Tunajua kuwa Simba wanaongoza Ligi na hapa ni ngome yao lakini tutawashangangaza kwa jinsi tulivyojiandaa kwani tumedhamiria kuchukua alama zote tatu tukianza na mchezo wa leo dhidi ya Simba,” amesema Shija
Nahodha wa Dodoma Jiji FC, Mbwana Bakari Kibacha amesema kuwa, wachezaji wote wapo vizuri na imara kuhakikisha wanatimiuza maagizo waliyotoka nayo Dodoma hivyo mashabiki wao watarajie mambo mazuri.
Kibacha amesema, wanawajua vizuri wapinzani wao Simba na benchi lao la ufundi limeshafanyia kazi makosa yote waliyoyaona kwa wapinzani wao kwani ikiwa watakuwa bora basi Simba hawawezi kuwa bora hivyo hawatajali ukubwa wa majina ya wachezaji wao kwani jukumu lao ni kushinda kila mchezo ulio mbele yao.
More Stories
15 wajinoa Juventus,akiwemo mtoto wa Mwenyekiti wa CCM Mbeya
Za Kwetu Fashion Show, yawapaisha wanamitindo nchini
TCAA yaadhimisha siku ya usafiri wa anga Duniani kwa kushiriki mbio za Marathon UDSM