November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yalipa maelekezo Jeshi la Polisi

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline, Kilimanjaro

NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Daniel Sillo ametoa maelekezo matano kwa Jeshi la Polisi ambapo amewasihi kuimarisha nidhamu, kwa Jeshi la Polisi, kuimarisha usalama wakati wa chaguzi zijazo, kuendelea kudhibiti ajali za barabarani, kuboresha mazingira ya Polisi ngazi ya kata/shehiya pamoja na kuendelea kutekeleza mapendekezo ya Haki Jinai nchini

Sillo amezungumza hayo kwenye halfa ya ufunguzi wa mkutano mkuu wa Maafisa Wakuu Waandamizi wa Jeshi la Polisi yaliyofanyika katika Shule ya Polisi Tanzania (TPS) Moshi,  mkoani Kilimanjaro Septemba 12, 2024

Sillo alilitaka Jeshi la Polisi kuendelea kuimarisha maadili na nidhamu kwa kuwa Jeshi lisilokuwa na nidhamu haliwezi kutoa huduma bora kwa wananchi na kwa watendaji wake

“Nisisitize kuendelea kuimarisha maadili ndani ya ya Jeshi la Polisi kwani nidhamu ndio msingi wa mafaniko katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku” Amesema Sillo

Pia alitumia fursa hiyo kuwapongeza Askari wote waliopandishwa vyeo na kuongeza kuwa hii inaonyesha ni kwa jinsi gani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyo na imani kubwa na Jeshi la Polisi

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Ally Gugu alilipongeza Jeshi la Polisi kwa kuendelea kuimarisha usalama wa raia pamoja na mali zao kwa kushirikiana na wadau mbalimbali pamoja na wananchi alitoa msisitizo kuwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi itaendelea kuratibu na kuwezesha majukumu ya Polisi kwa lengo la kuhakikisha Jeshi hilo linaendelea kutekeleza majukumu yake ipasavyo

IGP, Camilius Wambura alihitimisha kwa kusema Jeshi la Polisi limejiimarisha zaidi katika mkakati wa kuzuia uhalifu  alitoa rai kwa jamii kuhakikisha wanalea familia katika misingi na desturi nzuri za kitanzania ili kuepuka Mmomonyoko wa maadili ambao ndio chanzo cha uhalifu nchini.