December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

SIDO yaunga mkono jitihada za serikali kukuza viwanda nchini

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Mbeya

KAIMU Meneja wa Shirika la Viwanda Vidogo na Vya Kati (SIDO) Mkoa wa Mbeya Salma Galasi amesema,Shirika hilo linaunga mkono Kauli mbiu ya mwaka huu ya Manonyesho ya Wakulima Nane Nane kwa kuhakikisha wanatoa kipaumbele cha kuzalisha mashine za uchakataji mazao ya kilimo ili kumpunguzia adha mkulima kuanzia hatua ya kulima mpaka anapopaki mazao yake.

Kaulimbiu ya maonyesho ya Nane Nane mwaka huu ni Vijana na Wanawake Nguvu Imara katika kuleta Maendeleo ya Chakula .

Akizungumza na waandishi wa habari katika Banda la SIDO kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya,Galasi amesema,SIDO imekuwa iktekeleza kwa vitendo kaulimbiu hiyo ambapo kupitia kituo chao cha kuendeleza teknolojia ,wameweza kutengeneza mashine nyingi zinazohusika katika kilimo.

Aidha amesema,SIDO wamekuwa wakihudumia wajasiriamali mbalimbali lengo likiwa ni kupunguza umasikini na kuongeza kipato cha mwananchi mmoja mmoja.

“Katika dhana ya kuendeleza teknolojia tumekuwa tukitoa mafunzo hadi ngazi ya kijiji kwa vijana wanaohusika na utengezaji wa bunifu za kiteknolojia kwa kuwapatia mafunzo ,lakini pia tunazo programu za kuatamia kwa muda wa miaka mitatu ili kuwapa huduma ya mafunzo kwa ukaribu ili wafikie malengo yao na kuendeleza Tanzania ya viwanda.”amesema Galasi

Vile vile amesema wamekuwa wakitafuta masoko kwa ajili yawajasiriamali ndani na nje ya nchi kwa lengo la  kuhakikisha bidhaa zinazolishwa kuwa na soko la uhakika na hivyo kuwafanya wakulima kuongeza na tija katika uzalishaji na hivyo kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla.

Kwa mujibu wa Galasi,Shirika hilo pia limekuwa likitoa mafunzo kwa wakufunzi na wajasiriamali kama usindikaji vyakula ,utengenezaji bidhaa za ngozi,bidhaa za nguo lakini wamekuwa wakihusika katika kurasimisha biashara za wajasiriamali ambapo wamekuwa wakiwapa huduma za ugani kwa kuwatembelea katika meneo yao na kuwashauri njia bora za uzalishaji na kuwalea hadi kufikia hatua ya kupewa nembo za ubora TBS

“Hii yote ni kazi ya SIDO tunampokea mjasiriamali yule ambaye tu ana wazo la biashara na kuweza kumuongoza hadi kutekeleza wazo lake mpaka kwenye vitendo,pia baada ya kumpa mafunzo na kumuatamia tunampa mkopo ambao utamwezesha yeye kutekeleza wazo alilo nalo la kuweza kuzalisha bidhaa,

“Kwa hiyo SIDO tunamuunga mkono Rais wetu Dkt.Samia Suluhu Hassan kuhakikisha Tanzania ya Viwanda inafikiwa .”amesema