November 9, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Shule zatakiwa kubuni mikakati ya kudhibiti ajali za barabarani

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

SHULE nchini zimetakiwa kubuni na kutekeleza mikakati madhubuti ya kudhibiti ajali za barabarani kwa kuhakikisha zinatambua vihatarishi vilivyopo ndani na nje ya maeneo ya shule, pamoja na njia wanazotumia wanafunzi wanapokwenda na kurejea nyumbani.

Akizungumza katika hafla ya mashindano ya usalama barabarani yaliyodhaminiwa na kampuni ya TotalEnergies mkoani Dodoma, Afisa Taaluma wa Mkoa wa Dodoma, Mwalimu Justin Machela, amewataka wanafunzi kutumia maarifa wanayopata kutambua maeneo hatarishi na kutoa taarifa kwa walimu pamoja na watu wazima wanaohusika.

Amesema, “Wanafunzi wanapaswa kutumia maarifa wanayoyapata kutambua maeneo hatarishi na kutoa taarifa kwa walimu na watu wazima wanaohusika, badala ya kuchukua hatua zinazoweza kuhatarisha usalama wao.”

Katika mashindano ya mwaka huu mkoani Dodoma, Shule ya Sekondari Itega imeibuka mshindi mbele ya Shule za Sekondari Wella na Dodoma, na kujinyakulia zawadi ya Sh milioni 15 kwa ajili ya kuboresha mazingira ya usalama barabarani shuleni hapo.

Akizungumzia programu hiyo, Mkurugenzi wa Sheria wa TotalEnergies Marketing Tanzania Limited, Marsha Msuya, amesema tangu kuanzishwa kwake mwaka 2022, kampuni hiyo imetumia zaidi ya Sh milioni 400 katika kuendesha programu hiyo.

“Tangu kuanzishwa kwa programu hii mwaka 2022, tumetumia zaidi ya Sh milioni 400 katika kuimarisha elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi na jamii,” amesema Msuya.

Kwa upande wake, Sajenti Ester Makali kutoka Dawati la Elimu kwa Umma, Kikosi cha Usalama Barabarani cha Jeshi la Polisi, amesisitiza umuhimu wa elimu na ushirikiano katika kuimarisha usalama wa watumiaji wa barabara.

Ushindi huo umeiweka Shule ya Sekondari Itega katika nafasi ya kuiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya kikanda yatakayoshirikisha mataifa mbalimbali yakiwamo Uganda, Madagascar na Ivory Coast.