November 9, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mfuko wa Barabara kutumia bil.999.40

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online,Dodoma

MFUKO wa Barabara (RFB) unatarajia kutumia kiasi cha sh.bilioni 999.40 kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake muhimu, ikiwemo kugharamia miradi ya matengenezo ya barabara katika mikoa mbalimbali hapa nchini katika mwaka wa fedha 2026/27.

Kiasi hicho cha fedha kinatarajiwa kupatikana kupitia vyanzo mbalimbali vya mapato vinavyohusiana ikiwemo tozo za mafuta ya petrol na dizeli, tozo za magari ya kigeni yatumiayo barabara zetu pamoja na vyanzo vingine mbalimbali. 

Akizungumza wakati wa mahojiano maalumu na waandishi wa habari jijini Dodoma Kaimu Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mfuko wa Barabara, Mhandisi Rashid Kalimbaga amesema,sh.bilioni 816.34 zinatarajiwa kupatikana kutokana na makusanyo ya tozo ya mafuta, sh.bilioni 117.52 zitakusanywa kupitia tozo za magari ya kigeni yanayotumia barabara zetu (transit charges),huku kiasi cha sh.bilioni 65.52 zikitarajiwa kukusanywa kutoka vyanzo vingine mbalimbali.

Amesema,bajeti ya Bodi ya Mfuko wa Barabara iliyoidhinishwa kwa mwaka wa fedha 2026/27 ni sawa na asilimia 28 ya mahitaji yote ya fedha kwa ajili ya kuhudumia barabara za kitaifa na wilaya yaliyowasilishwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA).

“Chini ya bajeti hii, barabara ambazo kwa sasa ziko katika hali nzuri zimepewa kipaumbele, ambapo asilimia 100 ya fedha zinazohitajika kwa ajili ya matengenezo zimetengwa ili kuhakikisha barabara hizo zinaendelea kuwa katika hali nzuri na haziharibiki,”amesema.

Aidha, amesema kipaumbele cha matengenezo ya barabara hutolewa kwa barabara zenye kiwango kikubwa cha matumizi na zinazohudumia vituo muhimu vya kiuchumi, kijamii na kiutawala.

“Barabara hizo zinajumuisha korido kuu za kiuchumi za kitaifa kama TANZAM na Central Corridor, kwa kuwa zinahudumia bandari za Tanzania, pamoja na barabara zinazohudumia miji mikubwa, maeneo ya kilimo, vituo vya utalii na madini, maeneo ya viwanda, hospitali na vituo vya elimu,”amesema.

Amesema katika mwaka wa fedha uliopita wa 2025/26, Mfuko wa Barabara ulilenga kukusanya sh.bilioni 986.28 kutokana na tozo za mafuta na ushuru wa matumizi ya barabara huku ukifanikiwa kukusanya jumla ya sh.bilioni 1,221.23, sawa na asilimia 140 ya makadirio ya makusanyo yaliyokadiriwa.

Kuhusu tozo za magari yanayopita hapa nchini, amesema magari yenye ekseli hadi tatu hutozwa Dola za Marekani sita kwa kila kilomita 100, wakati magari yenye ekseli zaidi ya tatu hutozwa Dola 10 kwa kila kilomita 100.Kupitia tozo hizo watumiaji wa barabara wanachangia gharama za matengenezo ya barabara, hivyo kufidia uchakavu unaosababishwa na matumizi ya magari yao.

Hata hivyo,amesema kuwa Bodi inakabiliwa na changamoto mbalimbali katika ukusanyaji wa tozo na ushuru unaohusiana na miundombinu ya barabara. Alibainisha kuwa uwepo wa mifumo mingi ya kisheria pamoja na tafsiri tofauti za sheria hizo zinazotolewa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ni miongoni mwa changamoto zinazoathiri ukusanyaji wa mapato.

“Uwepo wa mifumo mingi ya kielektroniki ya usimamizi wa ukusanyaji wa mapato, pamoja na uwezo mdogo wa kifedha na kitaalamu wa kuwekeza katika vituo na maeneo ya kuzalisha mapato, kama vile maeneo maalumu ya maegesho ya malori, ni miongoni mwa changamoto nyingine zinazoathiri ukusanyaji wa tozo na ushuru unaohusiana na miundombinu ya barabara,”amebainisha.

Pia upungufu wa rasilimali watu ni changamoto nyingine inayoathiri usimamizi madhubuti wa ukusanyaji wa mapato katika mikoa yote hapa nchini.

Katika hatua nyingine, Bodi ya Mfuko wa Barabara imeziagiza TANROADS na TARURA kuandaa na kuwasilisha mikakati ya kuzuia au kupunguza uharibifu wa miundombinu ya barabara unaoweza kusababishwa na mvua kubwa za El-Nino zinazotarajiwa kuanza kunyesha karibuni.

Bodi pia imeziagiza Wakala za Barabara hapa nchini kuhakikisha miundombinu ya kupitisha maji, ikiwemo makaravati, inakuwa wazi ili kuruhusu maji kutiririka kwa uhuru huku wakiwashauri kutenga bajeti maalumu kwa ajili ya kugharamia kazi muhimu za dharura zitakazohitajika kurejesha ubora wa miundombinu ya barabara endapo kutatokea uharibifu wakati wa mvua.

Ameongeza kuwa, kwa mujibu wa sera ya Bodi ya Mfuko wa Barabara, kuhusu usimamizi wa kazi za dharura za matengenezo ya barabara, TANROADS na TARURA zinatakiwa kutenga asilimia tano ya bajeti zao kwa ajili ya kugharamia kazi hizo.Katika mwaka wa fedha 2026/27, jumla ya sh.bilioni 38 zimetengwa kwa ajili ya kugharamia kazi za dharura katika barabara za kitaifa na wilaya.

Amesema kuwa miongoni mwa malengo ambayo Bodi inalenga kuyafikia ili kuboresha ufanisi wa utendaji wake ni kuongeza matumizi ya teknolojia katika shughuli zake za kila siku na kuimarisha uwezo wa watumishi kupitia programu za mafunzo.