Na Joyce Kasiki,Timesmajira online ,Dodoma
Licha ya serikali kutatua changamoto ya vifaa vya kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi wasioona,lakini bado kundi hilo linakabiliwa na changamoto ya vitabu mguso hasa kwa darasa la awali ,darasa la kwanza na darasa la pili.
Akizungumza na mwandishi wetu , Mwalimu mkuu wa shule ya Msingi ya wasioona Buigiri iliyopo katika wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma Jonathan Samson amesema,kumekuwa na changamoto ya vitabu mguso shuleni hapo na hivyo kuathiri ujifunzaji kwa wanafunzi hasa wa darasa la awali ,darasa la kwanza na darasa la pili huku akisema upungufu wa vitabu va michoro mguso kwa makundi hayo upo kwa asilimia 75.
Amesema,upungufu huo ni changamoto kwa watoto kujifunza kutokana na ujifunzaji wao unategemea sana katika kuvitambua vitu au herufi kwa kugusa/kupapasa.
“Kama inavyofamika kwamba shule yetu pamoja na kuwa na wanafunzi wenye ulemavu wa aina nyingine,lakini pia wanafunzi walio wengi ni wale wasioona ambao kujifunza kwao ni kwa kugusa ,kwa hiyo tunapokuwa na uhaba wa vitabu mguso hasa kwa wale ‘bigginers’ (wanafunzi wanaoanza shule) inakuwa changamoto kubwa sana katika ujifunzaji wao.”amesema Mwalimu Samson
Aidha Samson ameiomba Serikali kuwashirikisha watu wasioona kwa asilimia 100 kuanzia wakati wa uandaaji wa michoro (vitabu vya michoro mguso ) na kuvifanyia majaribio ili washirikiane katika kuitambua michoro katika vitabu pindi tu vinapoandaliwa kwa lengo la kurahisisha ufundishaji na ujifunzaji wa watoto.
Ametumia nafasi hiyo kuiomba Serikali na wadau wengine wa Elimu kusaidia katika kuhakikisha changamoto hiyo inapata ufumbuzi hasa kwa mwaka ujao ambao serikali inaanza kutekeleza mtaala mpya.
Kwa upande wake Rehema John Mkazi wa Buigiri ameishukuru Serikali kwa namna inavyoshughulikia masuala ya watoto wenye ulemavu kwa kuhakikisha nao wanapata haki yao ya msingi ya kupata elimu huku akiiomba iendelee kuhakikisha inayaangalia makundi ya watoto wenye ulemavu na kushughulikia changamoto zao mapema kwani wengi wao wana uelewa wa taratibu.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Dkt.Semistatus Mashimba amesema katika kushughulikia changamoto hiyo,Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino ipo kwenye mazungumzo na wadau mbalimbali ikiwemo Wizara ya Elimu.
Kwa mujibu wa Programu Jumuishi ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto inayowalenga watoto wenye umri wa miaka sifuri hadi minane kuhakikisha kundi hili linafikia ukuaji timilifu ,uzoefu unaonyesha kuwa watoto wenye ulemavu wamekuwa wakitengwa kupata huduma muhimu kwa ukuaji wao.
Jema Chaula kutoka Ofisi ya Rais ,Tawala za Mikoa na Seriakali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia masuala ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto amesema,amelipokea na ataliwalisha eneo husika kwa ajili ya kufanyiwa kazi.
More Stories
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari