January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Shule 7 zapokea msaada wa madawati 170, miche 1,800 Ilemela

Na.Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza

TAASISI ya The Desk & Chair Foundation tawi la Tanzania limetoa msaada wa madawati 170 na miche 1,800 ya mbao,matunda na vivuli yaliyotolewa na taasisi hiyo kwa shule za Bwiru,Kitangiri C,Songambele, Amani,Isanzu,Kayenze na Nyamwilekelwa zilizopo wilayani Ilemela mkoani Mwanza.

Akizungumza wakati akipokea msaada huo kwa n Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela,Mariam Msengi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo,Hassan Masala,ameipongeza taasisi hiyo kwa jitihada za kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan za kutatua changamoto za elimu wilayani humo.


Msengi amesema serikali imeweka mkazo wa kuendeleza sekta ya elimu kwa kujenga miundombinu ya shule,hivyo inaipongeza na kuishukuru The Desk & Chair Foundation kwa kuguswa na wamekuwa mstari wa mbele kuipunguza changamoto ya elimu ambapo madawati hayo kila moja litakaliwa na watoto watatu.

“Ni jambo la kuenziwa,rai yangu kwa wanafunzi wa shule chache zilizonufaika na madawati hayo mkayatunze ili watakaokuja baadaye wayatumie kwani baadhi ya shule wenzenu wanakaa chini juu ya sakafu,hivyo serikali ikipata fedha itaendelea kutatua changamoto hiyo,”amesema Msengi.

Naye Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation,Alhaji Dk.Sibtain Meghjee amesema wanatekeleza miradi 45 maeneo mbalimbali ukiwemo wa ukarabati wa madawati wilayani Ukerewe.

Hivyo madawati hayo yatapunguza adha ya watoto kukaa chini wakiwa darasani katika shule za msingi za Kata ya Kirumba, Buswelu,Kitangiri,Kayenze,Bugogwa na Buzuruga.


“Gharama za madawati 170 na miche 1,800 ni milioni 23,zimetolewa na watalii vijana wanaosoma vyuo vikuu nchini Marekani mmoja akiwa mzaliwa wa Mwanza, waliomba waache athari chanya baada ya kutalii na walichagua kutoa madawati na visima sita vya maji,”amesema.

Alhaji Dk.Meghjee amesema kuwa miradi inayotumia mbao hupanda miti kufidia na kutunza mazingira ambapo miche 10 ni kwa dawati moja na kuzitaka shule zilizonufaika kupanda na kutunza miti hiyo hadi kuvunwa yakiwemo madawati hayo yaliyotengezwa kwa viwango vya ubora wa juu yasawasaidie muda mrefu.


Amesema msaada huo mbali na watalii wengine waliofadhili ni Aiden na Zara Ramji,Travon Muhhamad,Well Wishers na familia ya Tellis Foundation ambao ana uhakika wataendelea kusaidia kutatua changamoto za elimu zikiwemo za kijamii.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake John Daniel ameishukuru serikali kutoa elimu bure na The Desk & Chair kwa msaada wa madawati ambao utawapunguzia adha ya kukaa chini iliyosababisha baadhi kuandika hati mbaya huku Caren Pacshal akisema utaongeza ufaulu na kukuza taaluma.

Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii Manispaa ya Ilemela, Hussein Magera,amesema msaada wa madawati hayo 170 umeandika historia ya kupunguza sehemu kubwa ya kero ya madawati yanayohitajika,yataongeza ufanisi kwa wanafunzi kujifunza na walimu kufundisha.

Akizungumza kwa niaba ya Madiwani wa KKata za shule saba zilizonufaika,Diwani wa Kitangiri (CCM) Donald Ndaro amesema atakuwa mwizi na mtovu wa fadhila asipowashukuru The Desk & Chair Foundation kuwapunguzia aibu ya kukosa madawati pia kuwapa nafuu ya bajeti ya kuhudumia jamii.

“Nimewaona mkitoa misaada ya kijamii maeneo mbalimbali mkiunga mkono jitihada za Rais Samia za kumrua mama ndoo kichwani na kufanya kazi ya hamasa kwa watu wa nje.Ni akili ya ziada kutoa madawati na miche ya miti ili kurejesha uoto wa asili na mazingira,”amesema.

Awali Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Ilemela,Marco Isack,ameeleza wanao upungufu wa madawati 3,629 kati ya 26,444 ya mahitaji ya shule 83 za msingi,hivyo kupata hayo 170 bado wanahitaji 3,459 ambayo watayapunguza kwa fedha za mapato ya ndani kukidhi mahitaji ya shule hizo.
“The Desk & Chair Foundation kwa hili mlilofanya si jambo la rahisi,ni wachache wenye moyo wa kufanya hivi kama si moyo ya upendo wa Mungu pia,miti tuliyopewa tusipoitunza hatuwezi kupata madawati,hivyo twendeni tukailee ituletee manufaa baadaye,”amesema.