Na Mwandishi wetu,TimesmajiraOnline
HALMASHAURI ya Wilaya ya Mkinga imekusanya mapato ya sh.Mil.280 sawa na asilimia 94 kwa mwaka 2024/2025 kupitia shughuli za uvuvi.
Mapato hayo yamepatikana kutokana na uboreshwaji wa fukwe unaofanywa na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi na Mazingira na Uasili(IUCN) kupitia mradi wa Bahari Mali kushirikiana na wananchi kuunga mkono adhma ya serikali ya kukuza uchumi wa buluu nchini.
Akizungumza na wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania(JET), Ofisa Uvuvi wilaya ya Mkinga, Ezra Katete amesema mapato hayo yamekuwa yakiongezeka kila mwaka kutokana na mabadiliko mbalimbali yanayofanyika kwa kuboresha fukwe na kutoa elimu kwa wananchi wa eneo la Mkinga jinsi ya kunufaika na fursa za mazao ya bahari.
Katete amesema kupitia ushuru wa samaki wamekuwa wakikusanya sh. milioni 230 na leseni za uvuvi sh. milioni 45 na kusababisha kwa mwaka kukusanya sh. milioni 280 hadi sh.milioni 300 kwa mwaka kutokana na shughuli zitokanazo na uchumi wa buluu kama uvuvi.
Akizungumzia eneo la Mkinga wanayo bahari yenye urefu wa kilomita zaidi ya 71 ambayo ni urefu wa kutoka mpakani mwa Tanzania na Kenya na shughuli zinazofanyika ni uvuvi wa Samaki, pweza na samaki wadogo wa ukanda juu ya maji.
“Eneo la Mkinga lina jumla ya wavuvi 2,811 kwa mujibu wa sensa ya uvuvi iliyofanyika mwaka 2018, hivyo katika eneo hilo kumeonekana kuwepo kwa dalili za upungufu wa rasilimia hiyo kwa sababu idadi ya watu wanaotegemea bahari inaongezeka kila siku,” amesema
Amesema mwaka 2010 boti zilizokuwa zinavua samaki wadogo wa ukanda wa juu ya maji zilikuwa tano, sasa maboti makubwa yaliyosajiliwa ni 58 yapo mengine yanatoka Tanga na Dar es Salaam na kusababisja hali ya uhitaji kuongezeka.
Amesema wataalamu wa uvuvi wanategemea kuona shughuli zikiwa endelevu na katika kutekeleza hilo wamekuwa wakirejesha mazingira ya Bahari yaliyokuwa yameharibika kutokana na shughuli za kibinadamu kwa sababu awali kulikuwa na uvuvi mbaya wa baruti na kuharibu mazingira.
Amesema wamekuwa wakitengeneza matumbawe bandia na kutengeneza mengine mapya maeneo yaliyoathirika kuongeza uzalishaji wa samaki.
Katete amesema shirika la IUCN limekuwa msaada mkubwa kwao kwani wamekuwa wakisaidiana na wananchi kurejesha uoto wa asili ambao upo hatarini kupotea kama nyasibahari na mikoko.
“Kuna watu wamepanda mikoko kupitia miradi ya IUCN, kwa hiyo katika eneo letu kuna kazi zinafanyika, tunategemea tukiendelea hivi hali ya bahari yetu itarudi vizuri.
“Urejeshwaji wa nyasibahari utaongeza chakula cha samaki, eneo la nyasibahari linatumika kama sehemu ya mazalia au kujificha kwa samaki wengine adui asiweze kumuona wakazidi kuzaliana na kupunguza athari za hewa ukaa,” amesema
Katibu wa Kitengo cha Usimamizi wa Pwani (BMU) kijiji cha Moa, Mohamed Ndaro alisema katika shughuli za ulinzi wa rasilimali za bahari wamekuwa wakifanya uoteshaji wa mikoko, matumbawe, nyasibahari kulinda ikolojia ya bahari.
Pia kufanya doria kuangalia athari zinazosababishwa na binadamu na mabadiliko ya tabianchi.
Amesema jamii imekuwa ikishiriki kwa kiasi kikubwa kuotesha mikoko kwa sababu tayari imepatiwa elimu ya jinsi ya kutunza na kuipanda.
“Katika eneo la Mkinga wamebahatika kupata eneo kubwa lenye nyasibahari lakini kutokana na shughuli za kibinadamu zilizokuwa zikifanyika miaka ya 80 kuja 90 kuna shughuli za kibinadamu kama utumiaji wa baruti, kutumia nyavu za kuokota na kuathiri.
“Kuanzia mwaka jana kuna maeneo tumeanza kupanda lakini tulianza kukagua eneo kujua ukubwa, mafunzo kwa jamii ya uvuvi, mafundi wa vyombo vya bahari na wanufaika wa shughuli za bahari hivyo jamii imekuwa ikishiriki katika usimamizi na utunzaji kudhibiti wasiokuwa na nia njema,” amesema
Ndaro amesema baada ya urejeshwaji huo anatarajia kuona samaki, viumbe maji kuongezeka na ikolojia nyingine kuonekana baada ya uharibifu kupungua, shughuli za kibinadamu na utalii kuongezeka.
Kwa upande wake, Kwa upamde wake, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Moa, Sarah Mwaipasi amesema wamekuwa wakipata miradi mbalimbali kutoka kwa wafadhili juu ya utunzaji wa bahari na hususani kupanda nyasi bahari kuokoa uhai na ongezeko la samaki walioathiriwa kwa kukosa uoto wa asili.
“Utunzaji huo umetunufaisha wananchi kupata kipato kwa sababu wananchi wa MOA kwa asilimia 90 ambao ni 1,658 wanategemea shughuli zitokanazo na bahari,” amesema


More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako