January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

SHIVYAMAPIDA watoa msimamo wa kutoshiriki maandamano ya CHADEMA

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Shirikisho la waendesha bodaboda na bajaji Nchi Tanzania wametoa msimamo wa kutokushiriki maandamano ambayo yamepangwa kufanyika siku ya Septemba 23, 2024 Mkoani Dar Es Salaam yaliyotangazwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA.

Msimamo huo ulitolewa jana na Mwenyekiti wa Shirikisho la waendesha bodaboda na bajaji kwaniaba ya wanachama wote Nchini, Said Kagomba  na kusema kuwa tunu ya amani ya Nchi ni kubwa kuliko kitu chochote hivyo hawawezi kuishi kwa wasiwasi endapo wataandamana hawataweza kuthamini mali zao.

“Waendesha bodaboda na bajaji wa mkoa wa Dar es Salaam na Taifa kwa ujumla hatutoshiriki katika maandamano hayo . Tunu ya amani yetu ni kubwa sana leo hii sisi kama wasafirishaji utakapotokea uvunjifu wa amani sidhani kama tutaweza kumbeba abiria yoyote wa kuweza kumsafirisha kwenda sehemu nyingine pia tunaweza tukaishi kwa wasiwasi”



Aliwataka bodaboda wote na bajaji kwa siku ya tarehe 23 waendelee na utaratibu wao wa kufanya kazi, wasishiriki katika mambo yoyote yanayopelekea kuvunja amani ya Tanzania 

Alipongeza jitihada za Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada alizozichukua kuwapa maelekezo makamishna ya nini kifanyike lakini pia maelekezo ya maridhiano .



Pia Katibu wa Shirikisho hilo Michael Liganya amesema wakishiriki maandamano hayo watakuwa wametengeneza matatizo makubwa kwa sasa katika Nchi ya Tanzania bodaboda hawapo tayari kuwa miongoni mwa wavunjifu wa amani.



Aidha msemaji wa Shirikisho la waendesha bodaboda na bajaji Tito Lazaro amesema hakuna bodaboda atakae andamana siku ya Septemba 23 hivyo wataendelea na shughuli zao za kila siku zinazowawezesha kupata kipato na kuendesha maisha yao.

“Siku ya kesho bodaboda ukienda kuandamana na ukavunjwa miguu, ukivunjwa miguu utaendeshaje pikipiki na hii ndiyo ajira yetu, hakuna bodaboda wala bajaji atakayeandamana siku ya kesho bali siku hiyo ya maandamano sisi tutapiga kazi tu tupate kazi tukuze uchumi wa nchi”