Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online, Dar
CHUO cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimefanikiwa kuwawezesha wakufunzi kupata mafunzo ya kozi fupi kutoka Shirika La Kimataifa la Usafiri wa Anga Duniani (IATA).
Mafunzo hayo yalikuwa ni ya wiki sita kuanzia Septemba 28, 2020 hadi Novemba 4, mwaka huu kwa lengo la kuwajengea uwezo wakufunzi na pia wakufunzi kuweza kukidhi ubora wa viwango vya kimataifa.
Miongoni mwa wakufunzi wa NIT waliopata mafunzo hayo ni pamoja na marubani kutoka Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), Precision Air, Wakala wa Ndege wa Serikali, mamalaka ya usafiri wa anga na wahadhiri kutoka Shule Kuu ya Teknolojia ya Usafiri wa Anga ya NIT.
Kozi zilizosomwa na wakufunzi hao kuanzia Septemba 28 hadi Novemba 04 ni pamoja na Mfumo wa Usimamizi wa Ubora wa Unga (Quality Management System for Civil Aviation), Mbinu za Kufundisha (Instruction Techniques), Mfumo wa Usimamizi wa Usalama wa Anga (Safety Management System for Civil Aviation), Makosa ya kibinadamu (Human Factors), Ukaguzi katika masuala ya Anga (Aviation Internal Auditor) pamoja na Usimamizi wa Rasirimali na Utekelezaji katika Anga (Crew Resource Management and Implementation).
Hadi kumaliza kozi zote sita, wataalamu wa anga wapatao 150 wamenufaika na mafunzo haya yaliyotolewa hapa NIT. Haya ni mafanikio makubwa sana katika kuhakikisha mafunzo ya taaluma ya anga yanaendeshwa katika ubora unaokidhi viwango vya kimataifa.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye hafla ya kufunga mafunzo kwa kozi ya wakufunzi hao katika Kampasi Kuu ya NIT Mabibo jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Shule ya Teknolojia ya Usafiri wa Anga, Denis Mwageni alisema;
“Tumekamilisha mafunzo ya kozi fupi za IATA ambazo zilianza mnamo Septemba 28 hadi Novemba 4, 2020. Kwa sasa wakufunzi wetu wana uelewa mpana wa maeneo yote yaliyofundishwa ambayo pia ni muhimu sana kwa mujibu wa sheria na taratibu za Mamlaka ya Usafiri wa Anga ili kuweza kuendesha kozi za anga kwa ufanisi zaidi”.
Pamoja na mafunzo hayo, Mkuu huyo alisema; NIT tayari ni kituo cha IATA kiichoruhusiwa kufundisha kozi nne fupi za usafiri wa anga ambazo ni; Airline Marketing, Airline Customer Service, Airport Operations Fundamentals, global distribution systems fares na ticketing-Amadeus. Kozi hizi zitaanza kufundishwa mwaka huu wa masomo (2020/21) katika kampasi ya NIT Mabibo.
Mkuu wa Shule ya Teknolojia ya Usafiri wa Anga, Denis Mwageni anaendelea kusema: “Kozi za IATA tunazoanza kuzitoa ni fursa kwa Watanzania wote kwa sababu watazipata hapa NIT kwa gharama nafuu na pia kupata fursa ya ajira katika mashirika ya ndege ya ndani na kimataifa”.
Anaelezea kuwa lengo la Chuo cha Taifa Cha Usafirishaji ni pamoja na kuongeza kozi zaidi za IATA ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka katika sekta ya anga inayokua kwa kasi nchini.
“Mbali na kuanza kutoa kozi za IATA, NIT pia imepanga kuanza kutoa Shahada ya kwanza ya Uhandisi wa Matengenezo ya Ndege (Avionics) na Stashahada ya Uhandisi wa Matengenezo ya Ndege (Avionics) pamoja na kozi fupi za uhandisi mwaka huu ili kuwaanda wahandisi wasio na leseni waweza kufanya mitihani ya leseni,” amesema.
Akiongea wakati wa hafla ya ufungaji wa kozi hizo, Mkufunzi wa IATA kutoka Houston Texas, Marekani Andre aurelien aliwaambia wakufunzi waliopata mafunzo hayo kuwa jambo kubwa la kuzingatia katika sekta ya anga ni usalama kwanza.
Kwa upande wake, Naibu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma Utafiti na Ushauri Dkt. Prosper Mgaya alisema: “Tunayaomba Makampuni ya ndege ya ATCL, Precision Air na kampuni zingine kuleta hapa wafanyakazi wao kuja kusoma kozi hizi zilizoidhinishwa na IATA, kwani zitawasaidia katika kukuza na kuendesha vyema makampuni yao.”
Mmoja wa waliohudhuria mafunzo hayo Kapteni Hilal Fuad, kutoka Shirika la Ndege Tanzania-ATCL amesema:
“NIT imefanya uamuzi mzuri sana kuanza kutoa kozi hizi za IATA, kwa sababu zinatoa maarifa ya kina na ufahamu mkubwa katika tasnia ya anga. Kozi hizi zinakuongezea utaalamu zaidi.”
Naye, Kapteni Benjamin Maluli ambaye alihudhuria mafunzo hayo kutoka shirika la ndege la Precision Air amesema:
“Kozi hizi za kitaaluma ni chaguo bora kwa wanaotaka kwenda kufanya kazi ama wanaofanya kazi katika sekta ya anga, ninawashauri watanzania wenzangu waje kupata mafunzo haya hapa NIT.”
Mkuu wa Chuo Profesa Zacharia Mganilwa alisema hivi karibuni kuwa Taasisi iko katika hatua za mwisho za mchakato wa kutimiza taratibu zote za kuanza kwa kozi ya mafunzo ya marubani katika mwaka ujao wa masomo. NIT inasubiri ndege za mafunzo kuanza kutoa mafunzo hayo ya marubani.
Zaidi ya hayo, NIT imepokea U$ 21.25 milioni (takribani sh. bilioni) kutoka serikalini ikiwa ni mkopo kutoka Benki ya Dunia ili kusaidia kukuza mafunzo ya usafiri wa anga hapa nchini.
Shule ya Usafiri wa Anga na Teknolojia ya NIT ilianza kutoa kozi za Uhandisi wa Matengenezo ya Ndege mnamo 2015/16 Mwaka wa masomo. Wanafunzi 40 wamehitimu katika uhandisi wa matengenezo ya ndege ambapo 32 walipata shahada na wengine wanane walipata diploma. Wanafunzi 40 pia walihitimu katika programu ya wahudumu ndani ndege (cabin crew) tangu 2018 kozi hiyo ilipoanza.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
27 kulipwa kifuta jasho Nkasi
Mwakilishi Mkazi wa UN nchini awasilisha hati