Na Suleiman Abeid,Timesmajira Online, Shinyanga
Ukarabati wa kiwanja cha ndege cha Ibadakuli mkoani Shinyanga umeanza rasmi na unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi 18 kuanzia sasa ambao utagharimu zaidi ya milioni 49.
Hatua hiyo imepongezwa na wakazi wa Mkoa wa Shinyanga ambao wamesema kukamilika kwa kiwanja hicho kutaongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kwa wakazi wa mkoa huo na kurahisisha usafiri wa anga ikilinganishwa na hali ilivyo hivi sasa.
Mgeni rasmi katika uzinduzi wa kazi ya ukarabati huo Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Johari Samizi amesema kuanza kwa ukarabati wa kiwanja hicho umewapa matumaini makubwa wakazi wa Mkoa huo ambao kwa muda mrefu walikuwa wakipata shida ya kupata usafiri wa ndege.
Samizi amesema kuwa kiwanja hicho kitakapokamilika kitawaondolea wakazi wa Mkoa wa Shinyanga adha ya kusafiri umbali mrefu kilometa 164 kufuata huduma za usafiri wa anga jijini Mwanza na kuongeza fursa nyingi za kiuchumi kwa wakazi wake.
Hata hivyo amemtaka mkandarasi anayefanya kazi ya ukarabati huo, Kampuni ya China Hennan International Corparation Grp Co. Ltd (CHICO)kuhakikisha anatekeleza kazi hiyo kwa kiwango kinachokubalika kulingana na fedha ambayo imetolewa ya zaidi ya milioni 49.
“Kuanza kwa ukarabati huu kutamaliza kiu ya wakazi wa Mkoa wa Shinyanga ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa na shauku ya kuona kiwanja hiki kinaanza kufanya kazi,leo hii naamini wengi wamefurahi, kikubwa tuwaombe ndugu zetu wa Tanroads hakikisheni mradi huu unatekelezwa kwa wakati,” ameeleza Samizi.
Meneja wa Miradi ya viwanja vya ndege hapa nchini kutoka Tanroads Makao Makuu, Mhandisi Neema Joseph amesema kazi zitakazofanyika katika ukarabati huo ni pamoja na ujenzi wa barabara ya kutua na kurukia ndege kwa kiwango cha lami.Ukarabati wa barabara ya kuingi na maegesho ya ndege kwa kiwango cha lami, ujenzi wa jengo la abiria pamoja na (ATC), huduma za hali ya hewa na ujenzi wa barabara ya kuingia kiwanjani.
“Kazi nyingine zitakazofanyika ni ujenzi wa maegesho ya magari, ujenzi wa uzio wa usalama, ununuzi na usimikaji wa taa za kuongezea ndege (AGL), ununuzi na usimikaji wa mitambo ya usalama (DVOR/DME),mradi unatarajiwa kukamilika baada ya miezi 18 tangu tarehe ya kuanza,” ameeleza Joseph.
Kwa upande wake meneja wa Tanroads mkoani Shinyanga, Mhandisi Mibara Ndirimbi ametoa wito kwa wakazi wa mkoa wa Shinyanga hasa wale wa maeneo ambayo mradi huo unatekelezwa kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa kulinda miundombinu yote inayotumika kwenye kazi hiyo ya ukarabati.
Ndirimbi amesema,kuanza kwa utekelezaji wa ukarabati huu ni wazi wenyeji wa maeneo haya watapata fursa za ajira na hata mama lishe watapata fursa ya kufanya biashara, hivyo basi niwaombe sote tuwe walinzi wa mradi huu, pasiwepo na hujuma yoyote dhidi ya vifaa vya mradi.
“Kazi hii ni moja ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) hivyo tuhakikishe inatekelezwa bila matatizo, tujiepushe na vitendo vyoyote vya hujuma, mfano wizi wa mafuta, saruji au vifaa vyovyote vya ujenzi, mtu akiiba mjue anaihujumu Serikali siyo mkandarasi,”amesema.
Baadhi ya wageni waliohudhuria hafla hiyo fupi wameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza ahadi zake kwa vitendo ambapo wamemuomba mkandarasi ahakikishe anakamilisha kazi hiyo ndani ya muda uliopangwa na kwa kiwango kinachokubalika.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu