November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Shinyanga yaahidi ushirikiano utekelezaji wa Mama Samia Legal and Campaign

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme ameiahidi Wizara ya Katiba na Sheria na wadau inaoshirikiana nao katika kuendesha kampeni ya kitaifa ya msaada wa kisheria – Mama Samia Legal Aid Campaign kutoa ushirikiano wa hali na mali katika kufikia malengo ya kampeni hii ya kutoa msaada wa kisheria kwa watanzania wote hasa wale waishio maeneo ya pembezoni huku akiagiza kata zote zihakikishe zinanatenga maeneo maalum ambayo watoa huduma wataweza kuongea na mwananchi mmoja mmoja kwa faragha.

RC Mndeme ametoa kauli hiyo alipokuwa akihutubia kabla ya kuzindua rasmi utekelezaji wa kampeni hiyo mkoani Shinyanga hafla iliyofanyika katika viwanja vya Sabasaba Shinyanga mjini leo tarehe 11/06/2023 huku akiwaalika wakazi wote wa mkoa wa Shinyanga kushiriki Mama Samia Legal Aid Campaign itakayotolewa bure kwa wanachi katika Halmashauri zote sita kuanzia tarehe 11 – 21 Juni, 2023.


“Kwa mara nyingine tena, ninatoa wito kwamba sisi sote tushikamane katika kumuunga mkono Kiongozi wetu, Mama yetu, Mlezi wetu na Mtetezi wa Wananchi hususan wanyonge Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania katika kuondoa kadhia na viashiria vyote vya kuminya upatikanaji wa haki hususan ukatili wa Kijinsia kwa Wanawake na Watoto ambayo ndiyo changamoto kubwa ya Mkoa wa Shinyanga”. Amesema Mndeme

Mkuu wa Mkoa huyo ameongeza kuwa kampeni hii inatukumbusha watanzania wote uwajibikaji na usimamizi wa maamuzi yenye kuleta haki na akatumia fursa hiyo kuwambusha watumishi wote kutojihusisha na masuala ya rushwa inayopelekea kuzorotesha upatikanaji haki.

Aidha RC Mndeme amemuahidi Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa katika utekelezwaji wa Kampeni hii kwa kipindi
cha miaka mitatu, ofisi yake itasimamia maadili kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa haki kwa usawa.

Akitoa salaam na kumkaribisha Mgeni Rasmi, Naibu Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria Pauline Gekul amesema Wizara itaendelea kushirikiana na Mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar kuhakikisha Kampeni hiyo inatekelezwa ipasavyo ili kuwafikia watanzania kwenye Kata na Mitaa yote nchini.

Gekul amesema Wizara ya Katiba na Sheria inamshukuru Mhe. Rais kwa
kuendelea kudumisha utawala wa sheria; uzingatiwaji wa haki za binadamu na watu na kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wananchi wote lakini kwa jicho la kipekee kwa wananchi wasiokuwa na uwezo.

“Huduma ya msaada wa kisheria kuwafikia wananchi bure ni mapenzi na upendo
mkubwa wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mwananchi wa hali ya chini,”
amesema Gekul.

Akitoa maelezo ya awali kuhusu Mama Samia Legal Aid Campaign, Katibu Mkuu wa Katiba na Sheria Mary Makondo ametaja mafanikio ya kampeni hii toka ilipozinduliwa Mkoani Dodoma na kuendelea katika mkoa wa Manyara kuwa ni pamoja na kusuluhishwa kwa migogoro mingi ya kijamii na hata kifamilia iliyohusu ardhi iliyodumu miaka minne, mitano, na mwingine miaka kumi kulikopelekea watu hawa ambao walikuwa hawasalimiani na hata hawazikani kumaliza tofauti zao.

”Ziko familia ambazo wanafamilia walikuwa hawaongei kutokana na migogoro inayohusiana na ardhi, mirathi na sasa wamesuluhishwa katika Kampeni na wameungana katika kujenga familia zao na taifa kwa ujumla.” amesema Makondo.

Aidha Makondo amesema kwa kuwa kuna uwezekano mazingira ya mikoa hiyo kuwa sawa na Shinyanga hivyo uzoefu wa utatuzi wa migogoro hiyo utasaidia Kampeni hiyo kushughulikia masuala yote ya ukatili wa kijinsia, migogoro ya ardhi, mirathi na wosia na kuelimisha jamii kuhusu haki na wajibu wao wa kisheria na kikatiba kwa mbinu na uzoefu uliopatikana mikoa iliyotangulia na hivyo kuwezesha kampeni hiyo kufanyika kwa mafanikio makubwa zaidi katika mkoa wa Shinyanga.

Umuhimu wa kampeni hii ni wa kipekee katika kuongeza wigo wa ufikiwaji haki kwa wananchi, hususan walio vijijini na ambao hawawezi kumudu gharama za mawakili.

Kampeni hii pia imekuwa msingi mzuri wa kujenga uelewa wa wananchi kuhusu haki zao za kikatiba na kisheria; jambo ambalo ni muhimu katika kulinda na kukuza haki za binadamu nchini.

Hii ni kampeni ya miaka mitatu yenye lengo la kufikia mikoa yote nchini huku ikitarajiwa kuhitimishwa mwaka 2026.

Nae Meneja Rasilimali na Mawasiliano kutoka Shirika la Legal Services Facility (LSF), Jane Matinde amesema kuwa, uzinduzi wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia unakwenda kufanyika kila mkoa huku ukienda sambamba na utoaji wa huuduma
za msaada wa kisheria ili kuchochea upatikanaji wa haki kwa wananchi hasa wasiojiweza ikiwemo wanawake, watoto na makundi maalum.

”LSF tumekuwa tukishirikiana na Serikali kwenye kila ngazi kuwezesha upatikanaji wa haki kupitia utekelezaji wa programu ya upatikanaji haki. Tunafurahi kuona pia tumekuwa ni sehemu ya wadau muhimu katika utekelezaji wa kampeni hii nchini. Tunaahidi kuendelea kuwezesha wasaidizi wa kisheria kwenye kila ngazi ya wilaya ili kusaidia utoaji wa huduma za msaada wa kisheria bure kwa wananchi wote nchini,” amesema Matinde akimuwakilishi Makamu Mwenyekiti wa kampeni hii, Bi Lulu Ng’wanakilala ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa LSF.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Pauline Gekul akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa utekelezaji kampeni ya kitaifa ya huduma ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Mkoani Shinyanga.
Meneja Rasilimali na Mawasiliano LSF, Jane Matinde akizungumza kwa niaba ya Makamu Mwenyekiti wa kampeni ambaye Mkurugenzi Mtendaji wa Legal Services Facility (LSF), Lulu Ng’wanakilala wakati wa uzinduzi rasmi wa utekelezaji kampeni ya kitaifa ya huduma ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Mkoani Shinyanga.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme akitoa hotuba ya ufunguzi wakati wa uzinduzi rasmi wa utekelezaji kampeni ya kitaifa ya huduma ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Mkoani Shinyanga.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga akiwa ametembelea banda la maonyesho la wasaidizi wa kisheria wanaofadhiliwa na Legal Services Facility (LSF) wakati wa uzinduzi rasmi utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya huduma ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Mkoani Shinyanga.