Na Suleiman Abeid
Timesmajira Online, Shinyanga
WAKAZI wa Mjini Shinyanga wameadhimisha kumbukumbu ya miaka 24 ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kujitolea damu ili kuwasadia wahitaji mbalimbali hospitalini.
Wananchi hao wamesema suala la kuchangia damu ni muhimu ili kuweza kuokoa maisha ya wagonjwa wengi wanaohitaji damu wakiwemo wajawazito na watoto wanaofikishwa kwenye hospitali mbalimbali mkoani Shinyanga.
Wameyasema hayo wakati wakijitolea damu kwenye uwanja wa michezo wa CCM Kambarage Mjini Shinyanga ambapo wamedai baadhi yao huogopa kuchangia damu kwa kuhofia kupata madhara ya kimwili jambo ambalo si la kweli na kwamba utoaji damu mara kwa mara huwezesha mwili kuwa na afya njema wakati wote.
“Binafsi katika siku hii ya kumbukumbu ya kifo cha muasisi wa taifa letu Hayati mwalimu Julius Kambarage Nyerere nimeona ni vyema nikaitumia kwa kujitolea damu ambayo ninayoitoa leo hii inaweza kuwasaidia ndugu zetu mbalimbali wanaopatwa na matatizo mbalimbali ikiwemo ajali,”amesema.Godwin Ngetta.
Hata hivyo Godwin Ngetta ametoa wito kwa watanzania wengine wajitokeze mara kwa mara kuchangia damu maana hospitali zina mahitaji ya damu kutokana na uhitaji mkubwa uliopo pindi watu wanapopatwa na matatizo ikiwemo ajali za barabarani,wajawazito na watoto.
Ngetta ameiomba serikali kupitia Wizara ya Afya kukiongezea uwezo kitengo cha damu salama ambacho kina changamoto kubwa ya vitendea kazi ikiwemo usafiri wa kuwawezesha watendaji wake kufika maeneo ya vijijini kwa ajili ya kuhamasisha jamii kuchangia damu.
Ngetta amesema pamoja na umuhimu wa kitengo hicho bado Serikali imekisahau kukiwezesha ili kiweze kufanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa hasa upande wa hamasa kama inavyofanyika katika maeneo mengine ya uhamasishaji wa michezo ikiwemo ile ya mpira wa miguu na kubahatisha na hivyo watu wengi kujikita kwenye kufuatilia michezo hiyo.
Amesema ongezeko la vyombo vya moto hapa nchini ikiwemo pikipiki za kusafirisha abiria (bodaboda) limechangia kuongezeka kwa ajali za barabarani hali inayosababisha kuwa na uhitaji mkubwa wa damu.
Katibu wa CCM wa Kata ya Mjini Shinyanga Rashidi Abdalah ametoa wito kwa wananchi hasa vijana kujitokeza mara kwa mara kuchangia damu ili kuongeza akiba ya kutosha kwenye benki ya damu kwani mahitaji ya damu ni makubwa kwa sasa katika hospitali na vituo vingi vya afya nchini.
Kwa upande wake Mratibu wa Damu Salama Mkoa wa Shinyanga, Joel Mbale amewashukuru wananchi kwa kuonesha muamko mkubwa katika suala zima la kuchangia damu tofauti na hali ilivyokuwa huko nyuma ambapo nguvu kubwa ilitumika kuwaomba wananchi wajitolee damu.
“Kwa kweli hivi sasa wananchi wa Shinyanga wana muamko mzuri, mfano hapa leo hii tuna siku nne tayari tumekusanya units 426 lengo letu kwa wiki hii ya maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa ni kukusanya units 600, naamini tutafikia lengo,” ameeleza Mbale.
Kuhusu kumuenzi Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wananchi hao wameshauri watanzania waendelee kuyaenzi yale yote mema ambayo yaliasisiwa naye ambaye aliwaunganisha watanzania wote kuwa kitu kimoja bila kujali rangi, kabila wala dini zao.
Mwalimu John Tungu mkazi wa mjini Shinyanga amesema Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliiwezesha nchi yote ya Tanzania yenye makabila yapatayo 120 kuongea lugha moja ya Kiswahili na kuwafanya watanzania kuwa ndugu na nchi yao imeendelea kuwa na amani na utulivu mpaka hivi sasa tangu ijipatie uhuru wake kutoka kwa wakoloni.
“Amani na utulivu uliopo nchini hivi sasa ni moja ya tunu tuliyoachiwa na Baba wa Taifa, tunaishi vizuri bila vurugu zozote na Muungano wetu ni mfano katika mataifa ya Afrika japokuwa tuna changamoto ndogo ndogo za hapa na pale ikiwemo mmomonyoko wa maadili, ufisadi na rushwa, hivi vinapasa viachwe,”ameeleza Tungu.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi