Na Suleiman Abeid,Timesmajira Online, Shinyanga.
KATIKA kukabiliana na changamoto ya watoto wanaosoma shule za sekondari kutembea umbali mrefu kutoka vijijini kwenda shuleni Serikali mkoani Shinyanga inaendelea na mikakati mbalimbali ya kukabiliana na tatizo hilo.
Miongoni mwa mikakati ambayo inaendelea kuchukuliwa ni pamoja na ujenzi wa shule mpya za sekondari kwenye kata ambazo hazikuwa na shule hali iliyokuwa ina walazimu watoto wa kata hizo kusoma katika shule za kata jirani.
Kwa mujibu wa taarifa ambayo imetolewa na Ofisa Elimu wa Mkoa wa Shinyanga, Dafroza Ndalichako amesema mbali na ujenzi wa shule hizo zinazojengwa kupitia mradi wa SEQUIP pia wanajenga shule moja ya Mkoa ya bweni kwa ajili ya wasichana.
Ndalichako amesema mikakati inayochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na changamoto za umbali kutoka kijijini kwenda shuleni ni pamoja na kuendelea na ujenzi wa sekondari mpya katika kata ambazo hazikuwa na shule za sekondari.
“Mpaka sasa katika awamu ya kwanza Serikali imeishatumia zaidi ya bilioni 6 kujenga shule mpya saba za sekondari katika halmashauri zote zilizopo katika Mkoa wetu, ambazo ni Kagongwa, Ikinda, Bupigi, Igalamya, Lubaga, Shinyanga wasichana na Elias Kwandikwa,” anaeleza Ndalichako.
Anaendelea kueleza kuwa mikakati mingine ni kuongeza mabweni mapya katika shule za sekondari zilizopo ili kuongeza idadi ya wanafunzi wanaokaa bwenini ambapo kiasi cha cha zaidi ya bilioni 2, kinatarajiwa kutumika Serikali Kuu ikitoa zaidi ya milioni 865 huku kiasi kinachosaliwa kimetolewa na Barrick Bulyanhulu.
Hata hivyo hangamoto ya umbali wa shule za sekondari za kata imetajwa kuwa moja ya sababu ya watoto wa kike kutendewa vitendo vya ukatili na wengine kulazimika kukatisha masomo yao kwa hofu ya kufanyiwa vitendo hivyo ikiwemo kubakwa na kubebeshwa mimba zisizotarajiwa.
Baadhi ya wanafunzi wa kike wanaosoma kwenye shule za sekondari ambazo zimejengwa mbali na vijiji wanavyoishi wamekuwa wakiiomba Serikali iangalie uwezekano wa kuwajengea mabweni kwenye shule zao ili kuwaondolea changamoto ya kutembea umbali mrefu kila siku.
Neema Joseph (15) anayesoma shule ya sekondari Itwangi anasema yeye analazimika kutembea kilometa saba kila siku kwenda shule na kurudi nyumbani hivyo hutembea kilometa 14 kwenda na kurudi na mara nyingi anaporudi nyumbani hushindwa kujisomea kutokana na kupewa majukumu mengine ya kufanya ikiwemo kupika.
“Tunamuomba Rais Samia Suluhu Hassan atusaidie sisi watoto wa kike tunaosoma kwenye shule za sekondari hasa huku maeneo ya vijijini tunapata shida sana, shule nyingi ziko mbali na vijiji vyetu, tunalazimika kila siku kutembea umbali kwenda shule na kurudi nyumbani,”amesema na kuongeza kuwa
“Mfano mimi kila siku za masomo naamka saa 10 alfajiri ili kujiandaa kuja hapa shuleni, natembea kilometa saba na kurudi nyumbani inakuwa kilometa 14, njiani nakuwa peke yangu ni changamoto, lolote laweza kunitokea, hivyo iwapo tutajengewa hosteli hapa shuleni nitasoma kwa uhakika,” anaeleza Neema.
Mkuu wa shule ya sekondari ya Itwangi, Amos Stephen amekiri kuwa changamoto ya umbali wa shule ni moja ya sababu inayochangia watoto wengi kutokufanya vizuri katika masomo yao kushindwa kufuatilia masomo yao vizuri wawapo darasani kutokana na uchovu wa kutembea wanaokuwa wameupata wakati wakienda shuleni.
Kwa upande wao wakazi wa Kata ya Didia wanasema umbali wa shule za sekondari katika baadhi ya kata ni changamoto kwa watoto hasa wale wa kike na kwamba baadhi ya watoto mara nyingi hukwepa kwenda shule na kubaki mitaani wakicheza na jioni hurudi nyumbani wakisingizia walikuwa shule.
“Sisi hapa tulikaa na kushauriana jinsi gani tutatatua changamoto hii, bahati nzuri Serikali ilileta fedha kwa ajili ya kuongeza ujenzi kwenye sekondari mama ya Didia, tukaomba badala ya ujenzi uliotakiwa vyema tuanzishe ujenzi wa sekondari mpya ya Lohumba itakayokuwa karibu, tulikubaliwa,”
“Tumefanikiwa kujenga shule mpya ya sekondari iliyopo hapa hapa kwenye kata yetu ikiwa na vyumba vinne vya madarasa na tayari mwaka huu wanafunzi wameanza kusoma, tumeondoa ile changamoto ya watoto kutembea kilometa kumi kila siku kwenda kusoma kwenye sekondari ya Didia,” anaeleza Monica Mkolosi ofisa mtendaji kata ya Didia.
More Stories
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito